Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 22, 2026, anaondoka nchini kuelekea Addis Ababa, Ethiopia, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, itakayomuweka katika nafasi muhimu ya kushiriki juhudi za kikanda za kuboresha afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Akiwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Rais Dkt. Samia anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), pamoja na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika, utakaofanyika Novemba 23, 202
Mpango huo unalenga kuimarisha juhudi za nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kufikia malengo makuu matatu yanayofahamika kama Sifuri Tatu (Three Zeros), ambayo ni kuhakikisha kila mjamzito anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma za afya chini ya uangalizi wa mtaalamu, kutokomeza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kuhakikisha kila mtoto anapata huduma za chanjo.
Mpango Elekezi huo utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2026 hadi 2030, ukiwa na lengo la kuongeza uwekezaji wa Serikali za nchi wanachama na wadau wa maendeleo katika kuboresha huduma za afya, kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma bora na kuimarisha mifumo ya afya inayowahudumia wanawake, watoto na vijana barani Afrika.
Uzinduzi wa mpango huo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika na kuweka mwelekeo wa pamoja wa kukabiliana na changamoto za afya ya uzazi, mama na mtoto, hususan kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote.




Comments
Post a Comment