Na Sixmund Begashe, Iringa WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amezitaka taasisi za uhifadhi nchini, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kuongeza kasi ya kuhamasisha utalii wa ndani ili Watanzania waweze kunufaika moja kwa moja na matokeo chanya ya uhifadhi wa rasilimali za utalii. Dkt. Kijaji ametoa wito huo wakati wa kikao chake na menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na viongozi wakuu wa TANAPA na TAWA, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa mikakati ya kukuza sekta ya utalii nchini. Amesema kasi ya kuchechemua utalii na kuimarisha uhifadhi endelevu Kusini mwa Tanzania, inayotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, inapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo. Amebainisha kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa vivutio vya asili, hususan katika ukanda wa kusi...