Na John Mapepele Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kwa dhati kuisogeza Serikali karibu zaidi na wananchi wake hasa wale walio na kipato cha chini katika maeneo ya vijijini na mijini ili kuwaletea maendeleo. Akizungumza kwenye Kongamano la Uchumi la Arusha leo Mei 3, 2025 jijini Arusha akiwa miongoni mwa watoa mada, Mhe. Mchengerwa amefafanua kwamba lengo kuu ni kuwakomboa wananchi kutoka katika mnyororo wa ukosefu wa taarifa, huduma na fursa, kwa kuwajengea uelewa, uwezo na maarifa ya msingi, sambamba na kuwawekea miundombinu inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mipango yao ya maendeleo. “Tupo katika zama ambazo maendeleo hayategemei tena maamuzi ya viongozi wa kitaifa peke yao, bali yanategemea uwezo wa maeneo yetu ya mikoa na halmashauri zetu kuongoza kwa dira, maarifa na maamuzi ya kimkakati”...
Marato tv - Sauti ya Jamii