Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amezindua rasmi mfumo wa kisasa wa kidigitali wa Ngome SACCOS Limited, unaolenga kuboresha na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanachama. Uzinduzi huo umefanyika 19 Novemba, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Brigade Mess.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Nyansaho amepongeza uongozi wa Ngome SACCOS kwa kutumia teknolojia katika kuboresha huduma, akisisitiza kuwa Serikali inahimiza taasisi za fedha na vyama vya ushirika kuimarisha mifumo ya kidigitali ili kuongeza uwazi, kupunguza urasimu na kuwapatia wanachama huduma kwa haraka na ufanisi.
Mfumo huo unatarajiwa kupunguza matumizi ya karatasi, kuondoa makosa ya kibinadamu na kuimarisha usalama wa kumbukumbu za wanachama. Mwenyekiti wa Bodi ya Ngome SACCOS amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kujenga taasisi imara ya kifedha, yenye uwezo wa kukidhi ongezeko la wanachama na mahitaji ya huduma za mikopo kwa wakati na kwa viwango vya kisasa.
Wanachama waliohudhuria mkutano huo wameeleza matumaini yao kuwa mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa huduma bila kulazimika kusafiri umbali mrefu hadi ofisini, kwani sasa wataweza kuhudumiwa popote walipo. Uzinduzi huo unaashiria hatua muhimu katika mageuzi ya kiteknolojia yanayolenga kuongeza ufanisi na kuboresha huduma za kifedha kwa wanachama wa Ngome SACCOS.









Comments
Post a Comment