Kufuatia taarifa iliyochapishwa na chombo kimoja cha habari na kusambaa katika mitandao ya kijamii, ikidai kuwa walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba wameagizwa kuendelea kufundisha hadi Desemba 20, uchunguzi uliofanywa na George Marato TV umebaini kuwa taarifa hiyo si sahihi na haioneshi uhalisia wa utaratibu unaotekelezwa katika halmashauri hiyo.
Uchunguzi umebaini kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba haiendelezi shughuli za ufundishaji wakati wa likizo za shule, isipokuwa wanafunzi hupangiwa zamu maalumu za kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira ya shule pamoja na kuhudumia mashamba ya shule yanayozalisha chakula kwa ajili ya matumizi yao.
Aidha, taarifa iliyochapishwa na chombo hicho cha habari ilidai kuwa mdau mmoja wa elimu alikuwa ameitaka Idara ya Elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kuingilia kati agizo hilo linalodaiwa kutolewa, kuchunguza utaratibu wa malipo ya walimu na kuhakikisha walimu pamoja na wanafunzi wanapata likizo kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa kuhusu utaratibu wa halmashauri hiyo, hakuna agizo la kuendelea na ufundishaji wakati wa likizo, huku ikisisitizwa kuwa halmashauri inazingatia miongozo na taratibu zote za likizo zinazotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Kutokana na hali hiyo, taarifa zinazodai kuwa walimu wa Kwimba wamelazimishwa kuendelea kufundisha hadi Desemba 20 zinapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari, kwani zinaweza kuleta upotoshaji kwa jamii na kuibua taswira isiyo sahihi kuhusu usimamizi wa shughuli za elimu katika halmashauri hiyo.
Aidha, vyombo vya habari vimehimizwa kuzingatia misingi ya weledi na maadili ya uandishi wa habari kwa kuhakikisha taarifa zinazochapishwa zinathibitishwa kupitia mamlaka husika kabla ya kurushwa kwa umma, badala ya kutegemea taarifa zisizothibitishwa kutoka vyanzo visivyo rasmi.
Uhakiki wa taarifa kabla ya uchapishaji ni msingi muhimu wa kulinda uaminifu wa vyombo vya habari, kuzuia upotoshaji wa jamii na kuhakikisha umma unapata habari sahihi na zenye ukweli.




Comments
Post a Comment