SPIKA wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), leo Agosti 28, 2026, amepokea rasmi jina la Makamu wa Rais Mteule, Mhe. Deogratius John Ndejembi (Mb), lililopendekezwa na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa ajili ya kuthibitishwa na Bunge. Jina hilo limewasilishwa kwa Spika Zungu na Katibu wa Rais, Bal. Ali Jabir Mwadini, aliyeambatana na Mpambe wa Rais (ADC), Brig. Jen. Nyamburi Mashauri. Mapokezi ya jina hilo yameshuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari (Mb), pamoja na Katibu wa Bunge, Ndugu Baraka Leonard. Viongozi wengine walioshuhudia tukio hilo ni Wenyeviti wa Bunge, Mhe. Deogratius Mwanyika (Mb), Mhe. Najma Giga (Mb) na Mhe. Cecilia Pareso (Mb). Mhe. Ndejembi amependekezwa kushika nafasi hiyo ya Makamu wa Rais na jina lake sasa limewasilishwa rasmi Bungeni kwa hatua ya kuthibitishwa kwa mujibu wa taratibu za kikatiba.
Marato tv - Sauti ya Jamii