📍Wamasai wampongeza kwa Kasi ya miradi ya maendeleo
Na Mashaka Mhando, Korogwe
WANANCHI wa Kijiji cha Nanyogie, kilichopo Kata ya Mkomamazi wilayani hapa, wamempokea kwa shangwe na heshima kubwa Mbunge wao, Mhe. Timotheo Mnzava, kufuatia kimbunga cha maendeleo alichokiwasilisha kijijini hapo kinacholenga kugusa sekta mbalimbali za maisha yao ya kila siku.
Kijiji cha Nanyogie ambacho idadi kubwa ya wananchi wake ni wafugaji wa kabila la Kimasai, kipo Kusini, Mashariki pembezoni mwa mto Pangani.
Katika ziara hiyo iliyoacha alama kubwa, Mbunge huyo amewasihi wananchi wa jamii ya Kimasai kuhakikisha wanawapeleka shuleni watoto wao wote 13 waliofaulu mitihani ya darasa la saba ili kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, akisisitiza kuwa elimu ndiyo urithi pekee wa kuaminika kwa vizazi vijavyo.
"Serikali imejenga shule za sekondari karibu katika kila kata ili kuwawezesha watoto wetu kupata elimu bora. Hivyo, niwaombe kuhakikisha watoto wenu wote wanakwenda shule, na ikitokea changamoto yoyote ile, mnitie shime mimi na diwani wenu ili tusaidiane kuitatua," alisisitiza Mnzava, ambaye ni miongoni mwa wabunge mahiri mkoani Tanga wanaotajwa kwa utendaji kazi wa karibu na wananchi.
Aidha, akijibu kero na maombi yaliyowasilishwa na wananchi hao, Mbunge huyo alifanya maamuzi ya papo hapo kwa kutoa mikono ya kusaidia miradi ya jamii na taasisi za kidini, ambapo alitoa kiasi cha Shilingi 250,000/- zilizosaidia kununua mabomba ili kukamilisha mradi mdogo wa maji kijijini hapo na kuwaondolea wakazi adha ya kutembea umbali mrefu.
Katika sekta ya elimu, alitoa mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya kusakafia madarasa mawili ya Shule ya Msingi Nanyogie ili kuweka mazingira safi na salama ya kujifunzia, sambamba na kukabidhi Shilingi 200,000/- kwa uongozi wa Kanisa la KKKT kijijini hapo ili kulipia deni la dayosisi lililokuwa likiwakabili.
Pia, Mhe. Mnzava amewaahidi wananchi hao kuwa wakianzisha ujenzi wa jengo la kliniki ya Mama na Mtoto, yeye atachangia tofali 1,000 na kuisukuma serikali kuunga mkono juhudi zao, huku akihitimisha kwa kukabidhi jezi na mipira kwa vijana ili kuhamasisha michezo, burudani na mshikamano miongoni mwao.
Hata hivyo, wakazi wa kijiji hicho walitumia fursa hiyo kumshukuru kwa dhati Mhe. Mnzava na serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta unafuu mkubwa kupitia ujenzi wa kivuko cha daraja la muda mfupi, uboreshaji wa huduma za maji, umeme, elimu, afya, miundombinu ya barabara, na upatikanaji wa chanjo za mifugo kwa ajili ya kuendeleza ufugaji wa kisasa na wenye tija.
Mwisho





Comments
Post a Comment