Arusha, Oktoba 8, 2026
Wabunge kutoka Kundi la Kijiografia-Kisiasa la Bara la Afrika kupitia Umoja wa Mabunge ya Duniani (IPU) wameunga mkono ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana barani Afrika.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Arusha katika mkutano wa pembezoni wa Mkutano wa 153 wa IPU, ambapo viongozi hao pamoja na wadau wa maendeleo ya Sekya ya Afya Duniani wamejadili umuhimu wa kuimarisha sera, mifumo ya utoaji huduma, uwekezaji na uwajibikaji katika sekta ya afya.
Kiongozi wa Kundi la Kijiografia-Kisiasa la Wabunge wa Bara la Afrika kupitia IPU, Mhe. Ali Kolotou Tchaïmi, amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuunganisha nguvu, kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kuwa na agenda ya pamoja ya kuboresha afya ya mama na mtoto.
Kwa Upande wae Rais wa Umoja wa Mabunge ya Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema juhudi za Rais Samia katika kuimarisha afya ya uzazi zinapaswa kuungwa mkono, huku akisisitiza kuwa bila utashi wa kisiasa na uwajibikaji wa viongozi, wataalamu wa afya na na mifumo ya afya haitoshi kuimarisha Huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto.
“IPU inajidhatiti kuwa mshirika wa vitendo kwa mabunge katika kuhakikisha ahadi zinatafsiriwa kuwa hatua na matokeo chanya ya kuimarisha Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto” amesema Dkt. Tulia.
Naye Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema afya ya mama na mtoto ni kipaumbele cha Serikali ya Tanzania na kwamba Bunge kwa niaba ya wananchi lina wajibu wa kusimamia rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya huduma hizo.Awali, Mshauri wa Rais kuhusu Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema vifo vitokanavyo na uzazi barani Afrika vimepungua kwa asilimia 42 kati ya mwaka 2000 na 2023, lakini Afrika bado inachangia asilimia 70 ya vifo vya kina mama duniani.
Amesema kupitia Mpango Kazi wa Rais Samia wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Barani Afrika 2026–2030, ajenda ya Rais Samia inalenga kufikia Sifuri Tatu: sifuri ya kujifungulia nyumbani, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto, na sifuri ya watoto wasiochanjwa.
Kwa pamoja, wabunge na wadau wa afya wameonesha dhamira ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa hatua zinazolenga kuboresha afya ya wanawake, watoto na vijana barani Afrika na kufikia malengo ya mwaka 2030.









Comments
Post a Comment