TUMERIDHIKAAA
<Ni kauli ya Kamati ya Bunge baada ya kujiridhisha na maendeleo ujenzi wa miradi ya Umwagiliaji
<Yawataka wananchi kuchangia ada, yasisitiza wanarudi Bungeni kuibana Serikali
NA MWANDISHI WETU; SINGIDA
Kasi ya ujenzi wa miradi ya Umwagiliaji imewaridhisha Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara ya kamati katika skimu za Umwagiliaji , skimu ya Masimba na Msingi Mkoani Singida Mwenyekiti wa Kamati ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Mjini, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika, amesema wameridhika na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo.
Mwanyika amesema, kutokana na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya miradi ya Umwagiliaji inavyoendelea kamati itaenda kulieleza Bunge na kutoa msukumo kwa Serikali ili iweze kutoa fedha na kukamilika kwa wakati.
"Hatuna la kusema 'Tumeridhika' na ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji, tutaenda kuwapigania Bungeni tumepata nguvu ya kwenda kuwaombea fedha ili miradi hii mizuri inayogusa maisha ya mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla iweze kukamilika,"amesema.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi hiyo na wanachangia ada ya huduma za Umwagiliaji.
"Wananchi huu mradi ni wetu uendelevu wa fedha kuja hapa ni wa kudumu,
kwa miongozo ya Wizara chini ya sheria ambazo zinasimamiwa na Bunge hii ada ni muhimu sana tulipe ili maboresho ya kazi iliyofanyika ikiwemo mifereji iweze kuwa ya kudumu,"amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo(Umwagiliaji na Zana za Kilimo), Athuman Kilundumya amesema ziara hiyo imekuwa na tija na Wizara imeona Kamati hiyo ilivyo na nia ya kuijua miradi ya Umwagiliaji na Serikali ipo tayari kusimamia maelekezo ya Bunge.
"Mmeona ubora wa kazi zilizofanyika na miradi mliyotembelea baadhi inatekelezwa na wakandarasi wa ndani na Tume imekuwa ikiisimamia ipasavyo kwa kushirikiana na Wizara ili kuweza kupata thamani ya fedha,"alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa ameihakikishia Kamati hiyo ya Bunge kuwa ujenzi wa miradi ya Umwagiliaji inaenda kwa kasi na itaendelea kuleta tabasamu kwa wananchi.
"Miradi ya Umwagiliaji inakwenda kwa kasi na itaacha tabasamu kwa wananchi kama Rais alivyoelekeza, Tume tumefarijika na ujio wenu na tutahakikisha mnatembelea miradi mingine. Amesema Miradi inayotekelezwa ni zaidi ya 146 na kati ya hiyo asilimia 70 wakandarasi wake ni Watanzania hivyo Tume inatekeleza kwa asilimia 100 lengo la Serikali kuwezesha wakandarasi wazawa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Hajjat Asia Messos, amewataka wananchi wanaonufaika na miradi ya Umwagiliaji kuacha kuuza maeneo ili kufikia lengo la Serikali huku akisisitiza kuwa halmashauri hiyo imeanza kupima maeneo husika ili kupata mpango bora wa matumizi ya ardhi na tayari wamefanikiwa kuwafikia zaidi ya wananchi 200 na kupata hati za kilimo 900.















Comments
Post a Comment