Na Wellu Mtaki, Dodoma
SERIKALI imewataka waajiri kuacha mara moja tabia ya kutumia akaunti za watumishi wanaowasimamia kuomba mikopo binafsi bila ridhaa yao, ikieleza kuwa wanaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, jijini Dodoma wakati Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ukiwajengea uwezo maafisa rasilimali watu na wahasibu kutoka wizara na taasisi za umma nchini.
Mkomi amesema Serikali imeanza mchakato wa kuchunguza na kufuatilia mnyororo mzima wa waajiri wanaotumia taarifa au akaunti za watumishi wao kwa ajili ya kuomba mikopo binafsi bila kupata ridhaa ya wahusika.
Amesema vitendo hivyo ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za utumishi, huku akisisitiza kuwa Serikali haitawafumbia macho waajiri wanaowatumia watumishi wao kwa maslahi binafsi.
“Tunaanza kufuatilia mnyororo mzima wa waajiri wanaofanya mambo haya. Atakayebainika amevunja sheria na taratibu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema Mkomi.
Amesema matumizi ya akaunti za watumishi katika masuala ya mikopo bila ridhaa yao yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa watumishi, ikiwemo kuwaingiza katika madeni na majukumu ya kifedha ambayo hawakuyakubali.
Mkomi amesema suala hilo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito na waajiri kuhakikisha wanaheshimu haki, utu na maslahi ya watumishi wanaowaongoza.
WCF yatakiwa kuongeza wigo wa fidia
Katika hatua nyingine, Mkomi ameitaka WCF kuendelea kuangalia namna ya kupanua wigo wa fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhara mbalimbali kutokana na mazingira ya kazi.
Amesema kuna umuhimu wa kuangalia kwa mapana changamoto za kiafya zinazoweza kuwakabili wafanyakazi, ikiwemo magonjwa kama shinikizo la damu, ili kuona namna wafanyakazi hao wanavyoweza kupata msaada na huduma stahiki.
Aidha, amewaonya waajiri wanaowatelekeza watumishi wanapokuwa hospitalini baada ya kupata madhara, akisisitiza kuwa waajiri wana wajibu wa kuhakikisha taarifa zinawasilishwa katika maeneo husika kwa wakati ili wafanyakazi waweze kupata haki na msaada unaostahili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema shughuli zinazotekelezwa na mfuko huo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuhakikisha ustawi wa wananchi unakuwa jumuishi.
Dkt. Mduma amesema WCF inalenga kuhakikisha wafanyakazi wanaopata madhara kutokana na ajali au magonjwa yanayotokana na kazi hawasahauliki katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.
Amesema mfuko huo utaendelea kusimamia misingi ya ustawi, haki na usawa kwa wafanyakazi, akieleza kuwa misingi hiyo ni sehemu muhimu ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Lengo letu ni kuhakikisha mfanyakazi anayepata madhara yanayotokana na mazingira ya kazi anapata haki na huduma stahiki kwa wakati, ili asiwe nyuma katika kunufaika na maendeleo ya Taifa,” amesema Dkt. Mduma.








Comments
Post a Comment