Na Ssgt Mawazo Mtondo - DODOMA.
Kanda ya Magereza imeonesha uwezo mkubwa katika Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) 2026, baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kati ya Kanda saba zilizoshiriki mashindano hayo yaliyofanyika jijini Mwanza kuanzia Septemba 21 hadi Oktoba 3, 2026.
Kwa mujibu wa matokeo ya jumla yaliyotolewa leo, Oktoba 6, 2026, Kanda ya Magereza imefanya vizuri katika Mashindano ya BAMMATA 2026, baada ya kutwaa vikombe viwili vya mshindi wa kwanza kupitia michezo ya wavu kwa wanaume na wanawake, pamoja na vikombe vinne vya mshindi wa pili, vikiwemo mpira wa pete na kurusha vishale.
Aidha, Katika riadha, Kanda ya Magereza ilipata kikombe cha mshindi wa pili kupitia Inspekta Catherine Lange, aliyeshika nafasi ya pili katika mbio za Half Marathon.
Mafanikio hayo yanaonesha ushindani wa Kanda ya Magereza katika mashindano yaliyowakutanisha wanamichezo kutoka vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama nchini, kwa lengo la kuimarisha umoja, mshikamano, ushirikiano na uhusiano mwema kupitia michezo.
Katika msimamo wa jumla, Kanda ya Ngome iliongoza baada ya kutwaa vikombe saba vya nafasi ya kwanza, vitatu vya nafasi ya pili na viwili vya nafasi ya tatu, ikifuatiwa na SMZ iliyoshika nafasi ya pili kwa vikombe vitatu vya nafasi ya kwanza na vitatu vya nafasi ya tatu.
JKT ilimaliza nafasi ya nne ikiwa na kikombe kimoja cha nafasi ya kwanza, vitano vya nafasi ya pili na sita vya nafasi ya tatu, huku Polisi ikishika nafasi ya tano kwa kikombe kimoja cha nafasi ya kwanza, viwili vya nafasi ya pili na vinne vya nafasi ya tatu.
Zimamoto ilimaliza nafasi ya sita ikiwa na kikombe kimoja cha nafasi ya tatu na kutunukiwa Kombe la Ushiriki Mzuri katika Mashindano ya BAMMATA 2026 (Permanent Participation). Aidha, Uhamiaji ilitunukiwa Kombe la Mchezo wa Kiungwana (Fair Play) kwa kuonesha nidhamu, ustaarabu na mwenendo wa kiungwana katika kipindi chote cha mashindano hayo.











Comments
Post a Comment