Na Wellu Mtaki, Geita
SHIRIKISHO la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA) limesema moja ya mafanikio makubwa katika sekta ya madini ni kubadilika kwa mtazamo wa Watanzania kuhusu shughuli za uchimbaji, kutoka kwenye dhana za kishirikina na kuanza kuiona sekta hiyo kama shughuli inayohitaji sayansi, teknolojia na utaalamu.
Katibu wa Kamati ya Mahusiano wa FEMATA, Mathew Chengule, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Chengule amesema elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu sekta ya madini imekuwa na mchango mkubwa katika kuvunja dhana zilizokuwepo kwamba upatikanaji wa madini unahusishwa na uchawi au imani za kishirikina.
Amesema kwa sasa uelewa wa wananchi umeongezeka na wengi wameanza kutambua kuwa shughuli za madini zinahitaji matumizi ya teknolojia, taarifa sahihi na mbinu za kisayansi ili kuongeza ufanisi na kupunguza hasara.
“Hatua tuliyopiga ni kubwa sana. Cha kwanza tulichokifanya kama FEMATA ni kuwaelimisha Watanzania kwamba madini ni sayansi, siyo kama zamani ambavyo baadhi ya watu walifikiri kuwa ni uchawi au mambo mengine,” amesema.
Kwa mujibu wa Chengule, dhana hizo zilizokuwepo kwa muda mrefu ziliwafanya baadhi ya Watanzania kushindwa kutumia ipasavyo fursa zinazopatikana katika sekta ya madini.
Amesema juhudi za Serikali pamoja na vyama na taasisi zinazowakilisha wachimbaji katika kutoa elimu zimechangia kubadilisha mtazamo huo na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
“Tunashukuru Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na vyama vya wachimbaji kwa kutoa elimu kubwa sana. Sasa hivi tunaona madini yanaajiri Watanzania wengi,” amesema.
Amesema kuongezeka kwa uelewa kuhusu namna ya kutafuta maeneo yenye madini, kutumia teknolojia katika uchimbaji na kufanya biashara ya madini kumewahamasisha Watanzania wengi zaidi kuingia katika sekta hiyo.
Chengule amesema sekta ya madini inaendelea kuwa na nafasi katika kutoa ajira na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi, huku akieleza kuwa bado kuna fursa kubwa ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika miaka ijayo.
Amesema ili kufikia hatua hiyo, elimu kwa wachimbaji na wananchi inapaswa kuendelea sambamba na matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo katika sekta hiyo.
“Tunaamini tukifika hatua hiyo, sekta ya madini itaendelea kuwa chanzo kikubwa cha ajira na fursa kwa Watanzania,” amesema.

Comments
Post a Comment