ESAP MINING SERVICES YAIBUKA KINARA MAONESHO YA 9 YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA, YATWAA TUZO TATU KWA MPIGO
KAMPUNI ya Esap Mining Services Limited imetwaa tuzo tatu katika Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita, hatua inayotajwa kuwa chachu ya kuongeza ubunifu, matumizi ya teknolojia za kisasa na ufanisi katika shughuli za uchimbaji madini nchini.
Katika ushindi huo mkubwa, kampuni hiyo imejinyakulia tuzo za Mthamini Mkuu wa Maonyesho, Kampuni Bora ya Uchorongaji Miamba (Drilling) na mshindi wa pili katika kipengele cha Kampuni Bora ya Uchimbaji Madini.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo Leo Oktoba 2,2026 wakati wa Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Katika Viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan Mkoani Geita, Afisa Utawala na Mawasiliano wa Esap Mining Services Limited,ShabaniMitenenko Sadiki, alisema mafanikio hayo ni hamasa kwa kampuni kuendelea kuboresha huduma zake na kuongeza juhudi katika utekelezaji wa shughuli zake za uchimbaji madini.
Alisema kutambuliwa katika vipengele hivyo kunawapa ari ya kuendelea kutumia teknolojia za kisasa na kubuni mbinu zitakazoongeza ufanisi katika huduma wanazotoa kwa wadau wa sekta ya madini.
Sadiki pia aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka sera, sheria na kanuni zinazohimiza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi kupitia mfumo wa ushirikishwaji wa wazawa (Local Content).
Alisema hatua hizo zinatoa fursa kwa kampuni za Kitanzania kushiriki katika uwekezaji na kupata nafasi ya kutoa huduma mbalimbali ndani ya sekta ya madini, hivyo kuongeza ushiriki wa wazawa katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, aliwapongeza viongozi na wafanyakazi wa Esap Mining Services Limited kwa juhudi zao zilizochangia mafanikio hayo, huku akizitambua kampuni na wadau wanaoshirikiana nao katika shughuli za madini.
Miongoni mwa wadau hao ni Nyanzaga, Buckreef, Stamigold, Shanta Mining pamoja na wachimbaji wadogo wa madini nchini.
Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya kampuni za huduma za uchimbaji, wawekezaji na wachimbaji wadogo ni muhimu katika kuimarisha shughuli za sekta ya madini na kupanua fursa za biashara kwa kampuni za Kitanzania.
Mafanikio ya Esap Mining Services Limited katika maonyesho hayo yanaweka msisitizo katika nafasi ya ubunifu, teknolojia na ushirikiano wa wadau katika kukuza uwezo wa kampuni zinazotoa huduma katika sekta ya madini nchini.


Comments
Post a Comment