Askofu wa Kanisa la TGC, Robert Bundala amewataka wananchi kuiona Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii na si chombo kilicho mbali nao huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa dini, Polisi na wananchi ni muhimu katika kuimarisha amani na usalama.
Askofu Bundala ameyasema hayo Oktoba 08,2026 wakati wa ziara ya watumishi wa dini waliotembelea Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na kukabidhi mipira kwa ajili ya shughuli za michezo, hatua iliyolenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Polisi na jamii.
Amesema viongozi wa dini na Jeshi la Polisi wana majukumu yanayokaribiana katika kuelimisha jamii, kuzuia maovu na kuwasaidia watu kurejea katika mwenendo mwema.
Amesema viongozi wa dini wanashirikiana na Polisi katika masuala mbalimbali, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii na kushiriki katika kukemea uovu, shughuli za ulinzi na usalama, hususan katika maeneo ya nyumba za ibada.
“Polisi si watu waliotoka Mbinguni. Polisi ni ndugu zetu ni watoto wetu ni wadogo zetu na ni kaka zetu. Lakini wakati mwingine jamii huwaona Polisi kama watu walio mbali nao,” amesema Askofu Bundala.
Amesema mtazamo huo unaweza kuathiri ushirikiano kati ya wananchi na Polisi, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwa tayari kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kusaidia kuzuia na kukabiliana na uhalifu.
Kwa upande mwingine, Askofu Bundala amesema michezo ni miongoni mwa njia zinazoweza kuwaleta pamoja Polisi na wananchi, akieleza kuwa amekuwa akihusika katika kuratibu shughuli za michezo, ikiwemo Polisi Champion Cup, na kwamba uzoefu huo ulimfanya aone umuhimu wa kutumia michezo kuimarisha mahusiano.
Amesema utoaji wa mipira hiyo ni sehemu ya jitihada za kuunganisha jamii na Jeshi la Polisi kupitia michezo na shughuli nyingine zinazowakutanisha pamoja.
Ameeleza kuwa viongozi wa dini na Polisi wanafanya kazi inayofanana kwa namna tofauti, akitumia mfano wa viongozi wa dini kukemea dhambi na Polisi kukabiliana na vitendo vya uhalifu.
“Sisi tunakemea dhambi, ninyi mnakemea uhalifu. Wanaofanya dhambi watamchukia mchungaji anayewakemea na wanaofanya uhalifu watamchukia Polisi anayekabiliana nao. Kwa hiyo kazi yetu ni moja, tunaitenda kwa njia tofauti,” amesema.
Kwa upande wake, ACP Florence Mwenda, aliyezungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP. Wilbrod Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi linathamini ushirikiano na viongozi wa dini pamoja na jamii katika kuhakikisha amani na usalama unaendelea kuwepo.
ACP Mwenda amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa jukumu la ulinzi na usalama haliwezi kufanikiwa bila wananchi kuwa sehemu ya mchakato huo.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini, katika kutoa elimu kwa jamii, kuzuia uhalifu na kujenga mahusiano mazuri kati ya Polisi na wananchi.
Ameeleza kuwa michezo ni moja ya nyenzo zinazoweza kuimarisha mahusiano hayo kwa kuwa huwakutanisha watu katika mazingira ya kijamii na kujenga uaminifu na mawasiliano.







Comments
Post a Comment