Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

ASIYESIKIA LA MKUU HUVUNJIKA GU







 📍 Tujiadhari na mvua za Elni-nino

Na Mwajuma Selemani (Madam Nice) 0713689868

Ilikuwa mwaka 1993, nikiwa bado mtoto, katika Kijiji cha Jitengeni, Kata ya Mombo, Wilaya ya Korogwe Vijijini.

Kulikuwa na mvua za rasharasha zilizokuwa zikiendelea kunyesha kwa wiki hiyo. Kwa kweli, hazikuwa mvua kubwa sana za kutisha.

Ilikuwa asubuhi, mpiga mbiu alipoanza kutangaza:

“Tangazo! Tangazo! Tangazo!

Tunawatangazia watu wote katika Kijiji hiki cha Jitengeni kwamba kuna hatari ya kutokea mafuriko. Hivyo, tunaombwa tuondoke sisi pamoja na familia zetu.

Narudia tena: Asiyesikia la mkuu huvunjika guu, na mchelea mwana kulia hulia yeye.Serikali inawaomba sana wote mlioko mabondeni mhame mpaka hali itakapokuwa salama.”

Mpiga mbiu aliendelea kurudia tangazo hilo mara kadhaa. Hata alipokutana na mtu mmoja mmoja, alimsihi wahame.

Kwetu sisi, ilikuwa ni kama kupigia mbuzi gitaa, maana hakuna aliyemjali. Kila mtu alimpuuza.

Walioenda shambani kulinda mpunga waliendelea na shughuli zao. Wengine waliendelea na mihangaiko yao ya kila siku.

Mbiu ilirudiwa tena na tena, lakini watu waliipa kisogo. Wengine walimbeza na kusema kwamba amekosa kazi.

Muda ulizidi kwenda na mvua nayo ilizidi kuongezeka.

Kwa bahati nzuri, siku hiyo hatukwenda shule, hivyo wazazi hawakuwa na wasiwasi kuhusu watoto wao.

Kama kawaida yetu, kwa kuwa tuliishi karibu na mto, kila mvua iliponyesha tulikuwa tunaenda kuangalia kama maji yanaongezeka au la.

Tukaondoka watoto kama wanne hivi, tukaelekea mtoni. Tulipofika, kweli tuliyaona maji yakiongezeka kwa kasi.

Tukarudi kuwaambia wazazi:

“Mama! Mama! Maji yanaongezeka!”

Baba akasema:

“Bana, acheni kututishia nyau. Maji hayo, kwani hamjayazoea?”

Basi tukasema, “Mambo ya ngoswe tumuachie ngoswe mwenyewe,” kisha tukaenda kucheza.

Ilipofika saa 10 jioni, kelele za maji yaliyokuwa yakiongezeka ziliendelea kusikika katika kila nyumba.

Kwa kweli, hakuna aliyepata akili ya kuondoka na familia yake.

Badala yake, wazazi walichukua mijiti mikubwa na kwenda nayo mtoni. Lengo lilikuwa kuikita pembeni, mahali ambapo maji yalikuwa yanaishia, ili kuweka alama ya kiwango cha maji, baada ya kuikita ile miti, waliondoka.

Waliporudi, walikuta miti ile ilikuwa tayari imefukiwa na maji.

Gari la serikali la matangazo lilipita, likitutahadharisha kuhusu hali ya hatari na kututaka tuhame maeneo ya mabondeni. Lakini watu walikuwa kama wameziba pamba masikioni.

Wanakijiji wengi zaidi walitoka na kupiga kambi kandokando ya mto, wakistaajabu jinsi maji yalivyokuwa yakiongezeka kwa kasi.

Walishuhudia miti mikubwa na vitu mbalimbali vikisombwa na maji na kupita mbele yao, lakini hakuna wanakijij aliyegutuka.

Kutokana na mto kuwa mpana, maji hayakuweza kutoka kwa urahisi, hivyo watu wakajipa moyo kuwa hayawezi kutoka.

Muda ulizidi kuyoyoma na baadaye kiza kikapiga hodi.

Baada ya kiza kuingia, mioyo ya watu ilianza kutapatapa. Wasiwasi ukatanda kila mahali.

“Kama maji yatatoka, itakuwaje?” walijiuliza.

Lahaula! Maji yalianza kuchirizika taratibu kuelekea barabarani.

Kila mtu alitoka na kushuhudia maji hayo yakipita, kana kwamba hayana muda na watu. Na kama ujuavyo, sikio la kufa halisikii dawa. Hakuna aliyefikiria kuondoka.

Ilipofika saa mbili usiku, maji yalikuwa yanapita juu ya madaraja tuliyokuwa tunayatarajia kupita hivyo yakaziba njia zote za kutokea.

Hakukuwa tena na njia ya kutoka kuelekea upande wa pili ambao ulikuwa salama.

Bado watu walijipa moyo kwamba maji yangepungua.

Lakini maji yakawa ni kama yamechochewa.

Watoto tulichoka kusubiri, tukaingia ndani kulala, huku wazazi wakiendelea kuangalia maji yaliyokuwa yakipita nje.

Wakati tunaanza kunogewa na usingizi, maji yakapiga hodi ndani ya nyumba.

Yalivunja milango na kuingia kwa kasi kubwa.

Ama kweli, majuto ni mjukuu.

Wazazi walianza kuhaha.


Baba alianza kuondoa vitu na kuviweka sehemu za juu. Mama akakumbuka kwamba watoto walikuwa chumbani na maji yalikuwa yakijaa.


Mama alitukimbilia na kutuamsha.


Wakati huo, maji yalikuwa yamefika magotini.


Tulitoka kupitia mlango wa nyuma na kupandishwa kwenye sehemu yenye mwinuko kidogo.


Wakati maji yakiendelea kujaa, mama alikumbuka kwamba amemuacha mtoto wake mwingine wa mwisho ndani aitwaye hawa.


Bila kujali hali ya maji, alikimbia kuelekea chumbani huku maji yakimfika shingoni.


Alipofika, hakumkuta.


Akatoka kuelekea sebuleni akiwa amechanganyikiwa sana. Akapiga ukunga mzito:


“Mwananguuu!”


Lakini alijibiwa na mngurumo wa maji.


Wakati akiendelea kulia Mungu si Athumani!

Akakuta kitanda kinaelea juu ya maji, na mtoto akiwa juu ya godoro. Ilikuwa kama muujiza.


Sasa kazi ilikuwa ni kutoka pale na kurudi tulipokuwa sisi. akamueka mtoto kichwani huku maji yakimfika puani. Alipambana na maji mpaka akatufikia. .


Wakati wote huo, baba alikuwa akihangaika kujaribu kunusuru mali zake.


Tulikuwa na mali nyingi, ikiwemo makochi, televisheni, redio, vitanda, vyombo pamoja na magunia ya mpunga.


Magunia hayo ndiyo yaliyokuwa yaliyokuwa kitega uchumi cha baba. Lakini wakati huo hayakuwa na kazi tena; yalikuwa yamejaa matope na maji machafu.


Baba aliyatumia kama daraja ili kuweza kufikia na kuokoa baadhi ya vitu.


Sasa sebuleni kuligeuka kuwa bahari, hakuna tena aliyeweza kukanyaga sakafuni.


Maji yalipozidi watoto wote tukachukuliwa na kupandishwa juu ya paa la nyumba.


Kama kuna siku tuliwahi kuomba usiku uwe mfupi, basi ilikuwa ni siku hiyo.


Kumbuka, ulikuwa usiku wa manane.


Umeme ulikuwa umekatika kijiji kizima, giza lilikuwatotoro.


Hakukuwa na mawasiliano yoyote wala mtu wa kumuomba msaada.


 Vijiji vilivyoathirika vilikuwa vingi, hivyo waokoaji hawakuweza kutufikia kwa wakati.


Tukiwa juu ya bati, tulishuhudia watu wakibebwa na maji.


Wengine walikuwa wamekufa, na wengine walikuwa bado hai wakipiga kelele kuomba msaada, lakini hakuna aliyeweza kuhatarisha maisha yake kwenda kuwaokoa.


Tulishuhudia mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku ikisombwa na maji.


Mabunda ya fedha na vitu vilivyochukuliwa kutoka madukani vilikuwa vikielea na kupita mbele yetu.


Kwa kifupi, sasa kila kitu kilikuwa kama sinema.


Sinema ya mauti.

Sinema ya kutisha na kutia hofu.


Mvua ilizidi kunyesha na baridi kali ikapenya hadi kwenye mifupa.


Kila mtu alikuwa amelowa chapachapa.


Mioyo yetu ilizidi kupapatika tulipoona nyumba za jirani zetu zikibebwa na maji.


Yaani, nyumba zilibebwa nzima nzima, kana kwamba zilikuwa zimechimbuliwa na greda.


Baba yangu alikuwa amechanganyikiwa; hakujua afanye nini na aache nini.


Ama kweli, mfa maji haishi kutapatapa, na majuto ni mjukuu.


Tulijuta sana kwa kutowasikiliza viongozi wetu.


Watu waliosombwa na maji waliendelea kupita huku wakiomba msaada.


Nyumba nazo zilizidi kubebwa.


Hatimaye, kila mtu akabaki na Mungu wake, akisali na kulia.


Taratibu kulianza kucha.


Tukaanza kushuhudia helikopta za uokozi zikipita angani.


Zilipita na kutua katika Shule ya Msingi Jitengeni, ambayo kwa bahati nzuri haikupata madhara makubwa.


Waokoaji walianza kuwaokoa watu na kuwapeleka hapo. Lakini wengi walikuwa tayari wamepoteza maisha.


Manusura waliopelekwa hapo hawakuwa na chochote zaidi ya nguo walizokuwa wamevaa. Kila kitu kilikuwa kimebebwa na maji.


Hakukuwa na makazi ya kukaa.


Hakukuwa na chakula.


Wala mavazi ya ziada.


Tulimshukuru Mungu kwa kutuacha hai.


Tulianza kuwekewa mahema na kulala humo pamoja na magodoro.


Tukaanza kupanga foleni ya kugawiwa chakula, dawa na maji. Vyakula vingi vilikuwa tayari kwa ajili ya kuliwa na havikuhitaji kupikwa.


Tulilala humo mpaka kesho yake, tulipopewa msaada wa nguo, vyombo, vyakula na mahitaji mengine mbalimbali.


Ardhi ilipokauka, watu walirudi katika maeneo yao na kuanza kuchimbua, kusafisha na kujenga upya.


Kama ninapata nafasi ya kuishauri jamii inayoishi mabondeni au katika maeneo ambayo inajua yanaweza kufikiwa na maji, basi nawashauri sana waondoke kwa hiari yao wenyewe kabla ya hatari haijafika.


Kwani pilipili usiyoila huwezi kujua muwasho wake.


Kuna wakati utatamani upewe hata dakika tano za kuondoka, lakini utakuwa tayari umechelewa.


Kumbuka:


“Mchelea mwana kulia hulia yeye.”


Na pia:


“Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.”


Hili ni tukio nililolishuhudia nikiwa mtoto, lakini mpaka leo kumbukumbu yake bado iko hai akilini mwangu.


Mafuriko yale yalitufundisha jambo moja kubwa:

Wakati mwingine onyo linaweza kuonekana dogo, lakini madhara ya kulipuuza yanaweza kuwa makubwa kuliko tunavyofikiria.


Comments

#maratotv

RAIS RUTTO AAMBATANA NA ODINGA NCHINI CHINA

Rais wa Jamhuri ya Kenya Mh William Rutto na mke wake wamewasili nchini China kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali wa Jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). Katika ziara hiyo ameambatana na waziri mkuu mstaafu wa nchi hiyo Raila Odinga ambaye pia anapigiwa kampeni ili aweze kushinda nafasi ya Uenyekiti wa AU.

WIZARA YA MALI ASILI YASISITIZA MATUMIZI YA SHERIA NA KANUNI KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA UHIFADHI

Na.Joyce Ndunguru, Morogoro. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba asisitiza matumizi ya sheria na kanuni katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za uhifadhi. Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo leo Septemba 1, 2024 wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kuongea na watumishi ili kuimarisha utendaji kazi pamoja na kukagua maeneo ya kazi. "Kama wahifadhi tunapaswa kufahamu sheria zote zinazosimamia masuala ya uhifadhi zilizopo katika Taasisi zetu pamoja na za Taasisi zingine za uhifadhi zilizopo ndani ya Wizara ya Maliasili na utalii" amesema Kamishna Wakulyamba. "Pamoja na kufahamu sheria na kanuni zilizopo ndani ya Wizara yetu, ni vyema kufahamu na kuzingatia sheria nyingine za Nchi ambazo zinatuzunguka ili ziweze kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu mfano sheria inayohusiana na ukusanyaji wa vielelezo kuanzia kw...

Rais Dkt. Samia Awasili China Kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano Kati ya China na Africa FOCAC

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Beijing Capital nchini China kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) tarehe 03 Septemba, 2024.

MAKOMANDOO MIAKA 60 YA JWTZ,HAIJAWAHI KUTOKEA

Makomandoo ya jeshi la ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ)wamekuwa kivutio cha aina yake kwenye kikele cha maadhimisho ya miaka 60 ya tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo. Katika sherehe hizo ambazo zimefanyika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika uwanja huo wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 1 Septemba, 2024. Rais ameonesha kujivunia na kulipongeza JWTZ kwa kufanya kazi kwa kufuata misingi ya kuanzishwa kwake huku akitumia nafasi hiyo kuwapongeza Marais waliomtangulia kwa kazi kubwa waliyofanya wakati wa uongozi wao kwa kuliongoza vema jeshi hilo.

Meli ya Mv. Serengeti yapinduka na kuzama katika Bandari ya Mwanza kusini

 Meli Mv.Serengeti imepinduka na kuzama kwenye bandari ya mwanza kusini.  Meli hiyo imepinduka na kuzama disemba 26 majira ya saa Saba za usiku.  Tukio hilo limetokea meli hiyo ikiwa imefungwa katika gati la bandari ya mwanza kusini.  Kampuni ya meli Tanzania(Tashico) imethibitisha meli ya Mv. Serengeti kupinduka na kuzama upande mmoja wa nyuma.  Kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa na kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma cha Kampuni hiyo inaeleza kuwa Tashico imeshirikiana na Timu mbalimbali za Wataalam kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC), Mamlaka ya Usimamizi wa bandari (TPA) na wadau wengine katika Juhudi za Uokoaji.  Kwa Mujibu wa Taarifa hiyo,Taarifa rasmi ya chanzo cha Tatizo itatolewa Meli hiyo itakapokuwa imeinuliwa na Uchunguzi wa kubaini Tatizo utakapokuwa umefanyika. Meli ya Mv.Serengeti inadaiwa kusitisha safari zake kwenye ziwa Victoria mwaka 2016  Meli ya Mv.Serengeti imepinduka na kuzama katika...

Jenerali Jacob Mkunda Atembelea Meli Tiba ya China Aridhishwa na Huduma

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda ametembelea meli tiba ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China Peace Ark ili kuona matibabu yanavyofanyika. Jenerali Mkunda amefurahishwa na namna wataalam wa tiba wa Jeshi la China walivyotoa matibabu kwa kushirikiana na wataalam wa tiba wa JWTZ . Meli tiba ya jeshi la China imekuja hapa nchini na kutia nanga kwenye bandari ya Dar Es Salaam kutoa matibabu mbalimbali kwa wananchi ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa JWTZ  na ushirikiano wa miaka 60 baina ya JWTZ na Jeshi la Ukombozi la Watu wa  China. Matibabu hayo yalianza kutolewa tarehe 18 Julai 2024 hadi tarehe 22 Julai 2024. Meli tiba hiyo itaondoka hapa nchini tarehe 23 Julai mwaka huu.

AMIRI JESHI MKUU AKAGUA GWARIDE LA MIAKA 60 YA JWTZ

 Mapema leo asubuhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mhe.Dkt,Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride Maalumu la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Uwanja wa Uhuru leo September 01,2024. Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa jeshi la ulinzi la Wananchi Tanzania si jeshi la Uvamizi bali ni jeshi la ulinzi wa Wananchi Tanzania Amewahakikishia wanajeshi kufanya kazi kifua mbele,kuwa amiri jeshi mkuu yuko pamoja nao wakati wote.

Mbunge wa Bukoba Vijijini ameaga Sifa Kedekede Kwa Rais Samia

 Na Angela Sebastian; Bukoba  MBUNGE wa jimbo la Bukoba vijijini Dk. Jasson Rweikiza amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo, kwa kuwapatia zaidi ya shilingi bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mawili ambayo ni lango la kutoka na kuingia ndani ya mkoa wa Kagera. Ametoa shukrani hizo wakati akiongea wananchi mbalimbali waliofika katika viwanja vya Rweikiza pre and Primary school iliyoko eneo la Kyetema Bukoba vijijini, kwa kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa baba wa mbunge huyo aliyekuwa akiitwa Samsoni Rweikiza.  Rweikiza amebainisha kuwa,Dk. Samia Suluhu Hassan ni Rais mwenye upendo amekubali kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya Bukoba Vijijini na ndiyo maana tunasema atakuwa kiongozi wetu kwa awamu nyingine tena,tunapaswa kila mmoja kumuunga mkono. ametaja madaraja hayo kuwa ni Karebe ambalo limetengewa kiasi cha shilingi bil.9.3 kwa ajili ya ukarabati mkubwa kutokana na daraja ...

Jenerali ameacha alama ya uzalendo na kujitoa kwa ajili ya Taifa

*📌 Serikali itaenzi na kuthamini mchango wake* *📌 Asema Jenerali Musuguri alijitolea kuhakikisha Tanzania inabaki na amani na usalama* *📌 Asema alikuwa mstari wa mbele kuliokoa Taifa* *📌 Aiasa jamii kuacha alama katika maisha ya kila siku* *📌 Dkt. Biteko aongoza mamia ya watu mazishi ya Jenerali Musuguri Butiama* Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa  aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri alijitolea  kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa na amani, usalama na mshikamano pamoja na kuifundisha jamii  moyo wa dhati wa kuilinda nchi. Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 4, 2024 Butiama mkoani Mara wakati akiwasilisha salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Jenerali Mstaafu Musuguri. “ Katika  uhai wa kila mmoja wetu ni jambo gani mtu atakumbukwa nalo, baba huyu a...

Majaliwa Achangisha Shilingi Milioni 900 za Ujenzi wa Kanisa Kuu Lindi

  WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameendesha harambee na kuchangisha sh. milioni 928.67  za ujenzi wa kanisa kuu tarajiwa la Mt. Andrea Kagwa la Jimbo Katoliki la Lindi. Kati ya fedha hizo, sh. milioni 464.3 ni fedha taslimu na nyingine kati ya hizo zimeshawekwa benki na sh. milioni 464.37 bado ni ahadi. Awamu ya kwanza ya ujenzi huo, inatarajiwa kugharimu sh. milioni 700. Akizungumza na waumini na wadau mbalimbali waliohudhuria harambee iliyofanyika Ruangwa mjini, leo mchana (Jumamosi, Julai 27, 2024), Waziri Mkuu amewataka waliotoa ahadi wazikamilishe mapema ili kazi ya ujenzi isikwame. "Ninawashukuru sana wote mliofika na wote waliochangia ujenzi wa kanisa tarajiwa. Ninawaomba walioahidi, wakamilishe ahadi zao mapema ili kazi ianze kwani ramani ipo, mafundi wapo tayari,  wasimamizi wa ujenzi wapo," amesisitiza.  Waziri Mkuu amesema uamuzi wa Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa kuanza ujenzi wa kanisa kuu la jimbo hilo, ni utekelezaji ...