Na. Wellu Mtaki , Dodoma
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeeleza kuwa ushiriki wake katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita unalenga kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali kupata elimu na uelewa mpana kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia nchini.
Kupitia maonesho hayo, TPDC imeweka msisitizo katika kutoa taarifa sahihi kuhusu shughuli mbalimbali zinazohusiana na utafutaji, uchimbaji, uzalishaji na matumizi ya mafuta na gesi asilia, pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika maonesho hayo, Hassan Temba kutoka TPDC, amesema ushiriki wa shirika hilo ni sehemu ya juhudi za kuifikisha elimu ya mafuta na gesi asilia kwa wananchi kwa njia rahisi na inayoeleweka, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kufahamu namna rasilimali hizo zinavyotafutwa, kugunduliwa na kuendelezwa.
Amesema Tanzania imepiga hatua katika kugundua na kuendeleza rasilimali ya gesi asilia, hivyo wananchi wanapaswa kuwa na taarifa sahihi kuhusu sekta hiyo na mchango wake katika uchumi na maendeleo ya nchi.
“Tumepata fursa ya kuja katika maonesho haya ili kutoa fursa kwa wadau wote wanaofika hapa, pamoja na wale wanaotufuatilia, kuweza kujua shughuli zinazofanyika katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini,” amesema Temba.
Ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo, wananchi wanaweza kupata uelewa kuhusu hatua mbalimbali zinazopitiwa katika mchakato wa utafutaji na uchimbaji wa gesi asilia, kuanzia hatua za awali za utafiti hadi kufikia matumizi ya rasilimali hiyo.Kwa mujibu wa Temba, elimu hiyo ni muhimu kwa jamii kwa kuwa inasaidia wananchi kuelewa kwa undani namna rasilimali za mafuta na gesi asilia zinavyoweza kuchangia katika maendeleo ya Taifa na kutoa fursa mbalimbali kwa wadau wanaotaka kushiriki katika sekta hiyo.
Ameeleza kuwa TPDC inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali, ikiwemo maonesho, kuwa karibu na wananchi na wadau kwa ajili ya kutoa elimu, kujibu maswali na kuongeza uelewa kuhusu shughuli zinazofanywa katika sekta ya mafuta na gesi asilia.
Temba ametoa wito kwa wananchi, wanafunzi, wataalamu, wawekezaji na wadau wengine kutembelea banda la TPDC katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu mafuta na gesi asilia, teknolojia zinazotumika katika utafutaji na uchimbaji pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.
Maonesho hayo yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wananchi, wataalamu, taasisi na wadau mbalimbali katika kujifunza, kubadilishana uzoefu na kufahamu kwa karibu maendeleo ya teknolojia na matumizi ya rasilimali kwa ajili ya kukuza uchumi wa Tanzania.

Comments
Post a Comment