Na Mwandishi Wetu, Muheza
MBUNGE wa Jimbo la Muheza ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo, Hamis Mwinjuma (MwanaFA), ameongoza mamia ya wananchi wa mtaa wa Beach Boy, Kata ya Majengo, katika zoezi la uzoaji taka na kutoa udongo kwenye mfereji mkuu wa eneo hilo ili kukabiliana na tishio la mvua za El-Nino.
Katika zoezi hilo la msalagambo lililofabyika Leo Septemba 25, Mbunge huyo alishiriki moja kwa moja kutoa udongo uliokuwa umeziba mfereji huo ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi wakati mvua hizo zitakaponyesha, hatua itakayosaidia kuzuia maji kutuama na kusababisha mafuriko.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mwinjuma alisema lengo la usafi huo ni kuamsha ari ya kila mwananchi kuchukua jukumu la kusafisha mazingira yake kama hatua ya awali ya tahadhari.
"Kila mmoja afanye usafi katika eneo lake kwa sababu kuna tishio la mvua za El-Nino ambazo zinatarajiwa kuwa kubwa. Kila mmoja akichukua jukumu lake, uwezekano wa kutokea kwa maafa unakuwa mdogo sana," alisema Mwinjuma.
Pia, Mbunge huyo aliutaka uongozi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kutazama uwezekano wa kufanya ukarabati wa haraka kwenye karavati lililopo eneo hilo ili maji yapite moja kwa moja bila kukwama.
Vilevile, alishauri Halmashauri ya Wilaya kuweka mkakati wa kuwahamisha wananchi wanaoishi mabondeni na kuwapeleka maeneo salama, huku akisisitiza kusitishwa mara moja kwa utoaji wa vibali vya ujenzi kwenye maeneo hatarishi.
Akipokea maagizo hayo, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Muheza, Athanas Faris, alisema mpango wao kwenye eneo hilo ni kujenga kalavati la kisasa la zege (Box Culvert) ambalo litasaidia kupitisha maji kwa wingi na kuondoa kabisa kero ya mafuriko.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Muheza (DAS), Mohamed Mfaki, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, aliwasisitiza wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni na karibu na mifereji mikubwa kuchukua tahadhari mapema iwezekanavyo ili kuepusha uwezekano wa kutokea maafa.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Muheza, Simon Leng'ese, alishauri itolewe elimu ya kutosha kwa wananchi wa maeneo hayo ili waweze kujiokoa kabla ya maafa kutokea.
"Mvua zitakuwa kubwa, hivyo watu wote wanaokaa kwenye mabonde wachukue tahadhari za mvua hizo ili kuondoa uwezekano wa kutokea kwa mafuriko yatakayopoteza maisha na mali," alisisitiza Leng'ese.
Zoezi hilo lilihitimishwa na Diwani wa Kata ya Majengo, ambaye alitoa shukrani za dhati kwa wananchi wa kata yake na wale wa Kwamkabala kwa kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za Mbunge wao katika kufanya msalagambo huo.







Comments
Post a Comment