Na Mwanamkuu Mwandoro,Tanga.
Mamlaka ya Bima Tanzania 'TIRA' imesema kuwa inaendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa bahari wakiwemo wavuvi na wanaofanya shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo ili wawe na huduma ya bima itakayowasaidia pindi watakapopata majanga.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Kaskazini Dkt. Emmanuel Lupilya wakati alipokuwa akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa ujezi na uchukuzi David Kihenzile alipotembelea na kukagua Banda la Mamlaka hiyo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya usafiri majini Duniani iliyofanyika mkoani Tanga wakieleza namna walivyojipanga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na watumiaji wa bahari.
Dkt. Lupilya amesema kuwa lengo lao ni kuhakikisha kuwa mizigo yote ya ndani na nje ya nchi inayosafirishwa kupitia usafiri wa majini ikatiwe bima pamoja na vyombo vinavyo beba mizigo hiyo ikiwemo Mashua nahii itakuwa ni kinga itakayowasaidia pindi itakapotokea changamoto.
"Tunaendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa vyombo vya Majini vya kusafirishia mizigo na abira juu ya umuhimu wa kukata bima, pia tumejipanga kuhakikisha kwamba mizigo yote inayoingia iwe ya Tanzania au nje ya nchi na yenyewe ni lazima ikatiwe bima ili kukinga athari zinazoweza kujitokeza wakati wakifanya shughuli zao hili ni eneo ambalo tunakwenda kuliwekea msisitizo" amesema Dkt. Lupilya.
Aidha Meneja huyo ameipongeza Serikali kwa jinsi inayoendelea kuboresha miundombinu ya bahari pamoja na Bandari ikiwemo Bandari ya Tanga ambayo imeanza kuleta manufaa akisema kuwa maendeleo hayo yaendane na mabadiliko kwa jamii kupitia fursa zilizopo kwenye uchumi wa buluu .
Ameongeza kuwa TIRA imemfanya mazungumzo na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kushirikiana kwa lengo kuhakikisha kuwa vyombo vyote vya usafiri vinavyoingia hapa nchini viwe vimekatiwa bima hii ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya bima namba 394.
Akifunga maonesho hayo kitaifa kwa mwaka 2026 Naibu Waziri wa ujezi na uchukuzi David Kihenzile amesema kuwa sekta ya usafiri majini imekuwa ni kiungo muhimu kwa Tanzania na mataifa mengine ambapo zaidi ya nchi saba zinategemea kuchukua mizigo mbalimbali kutoka hapa nchini na kutumia usafiri wa majini
Pamoja na hayo pia ameongeza kuwa kulingana na takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania 'TRA' sekta ya usafiri na usafirishaji majini umekuwa ukichangia asilimia 40 ya Pato la Taifa.
Naibu Waziri huyo alimalizia Kwa kiwaagiza Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na wakala wa meli Zanzibar (ZMA) kuhakikisha zinaendelea kufanyanga ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vyombo vyote vinavyotumia usafiri huo ili kuepukana na changamoto ambazo zinaweza kujitokeza wawapo safarini.




Comments
Post a Comment