Na Wellu Mtaki, Geita
Jumuiya za mazingira zimeitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongeza na kuendeleza ushirikiano na wananchi katika kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi, huku zikitaka jamii kueleweshwa namna matumizi ya nishati hiyo yanavyoweza kuchangia katika utunzaji wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Chato mkoani Geita, Peter Lous, alipotembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya Tisa ya Madini yanayofanyika mkoani Geita ambapo TANESCO imewasilisha teknolojia mbalimbali, ikiwemo majiko yanayotumia umeme, yanayolenga kupunguza matumizi ya nishati zinazochangia uharibifu wa mazingira.
Lous amesema ushirikiano kati ya Serikali, taasisi na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha mipango ya nishati na mazingira inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Amesema wananchi wanahitaji kupewa elimu ya kutosha kuhusu teknolojia hizo ili waweze kuzifahamu, kuzitumia kwa usahihi na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kukabiliana na changamoto za mazingira.
“Tunawapongeza sana TANESCO kwa kazi nzuri wanayoifanya. Umeme ni muhimu kwa uzalishaji wa nchi, hivyo tunahitaji kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha huduma hii inapatikana kwa wananchi wengi zaidi,” amesema Lous.
Aidha, Lous amesema huduma bora na ya uhakika ya umeme ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na kuchochea maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa upatikanaji wa umeme unapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi.
Ametoa wito kwa wadau wa mazingira na wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kwa jamii na kutafuta suluhisho la changamoto zinazohusiana na mazingira na nishati.
Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Geita amesema kuanzishwa kwa makundi ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali kumewezesha wananchi kuwasilisha changamoto zao kwa urahisi na kupata majibu kwa wakati.
Amesema hatua hiyo imeongeza ushirikiano kati ya TANESCO na wananchi, huku baadhi ya changamoto ambazo hapo awali zilikuwa zikilalamikiwa mara kwa mara zikipungua.
Ameeleza kuwa mawasiliano ya karibu kati ya wananchi na shirika hilo yamekuwa muhimu katika kubaini changamoto za huduma za umeme na kuzifanyia kazi kwa wakati.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutumia njia zilizowekwa na TANESCO kuwasilisha changamoto zao ili ziweze kushughulikiwa kwa ufanisi.



Comments
Post a Comment