Na Angela Sebastian, Bukoba
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh2.7 bilioni kati ya Sh5.2 bilioni zilizokuwa zinadaiwa kutoka kwa kampuni binafsi 146 kwa ajili ya michango ya wafanyakazi wao katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Ismail Bukuku, amesema hayo Septemba 16, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba, akieleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya taasisi hiyo kufanya ufuatiliaji wa madeni ya michango ya wafanyakazi.
Bukuku amesema kampuni hizo zilikuwa hazijawasilisha michango ya wafanyakazi kwa kipindi cha miaka tisa, kuanzia mwaka 2017 hadi Julai 2026, hali iliyosababisha deni kufikia Sh5.2 bilioni.
Amesema katika awamu ya kwanza ya operesheni, TAKUKURU iliokoa Sh1.6 bilioni, sawa na asilimia 31 ya fedha zote zilizokuwa zinadaiwa.
Katika awamu ya pili, timu ya ufuatiliaji iliweza kuokoa zaidi ya Sh1 bilioni, hivyo kufanya jumla ya fedha zilizookolewa kufikia zaidi ya Sh2.7 bilioni, sawa na asilimia 52 ya deni lote.
Ameeleza kuwa operesheni hiyo ilifanyika kwa awamu mbili, ambapo ya kwanza ilikuwa kuanzia Julai 22 hadi Agosti 5, 2026, na ya pili kuanzia Agosti 17 hadi Agosti 31, 2026.
TAKUKURU imeendelea na ufuatiliaji wa kiasi cha fedha kilichosalia, kwa lengo la kuhakikisha kinapatikana kwa asilimia 100 na kuwasilishwa NSSF, ili kulinda haki za wafanyakazi na kuhakikisha wanapata mafao yao kwa mujibu wa taratibu.


Comments
Post a Comment