Kutokana na utabiri wa mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha nchini katika kipindi hiki cha mvua za El Niño, Diwani wa Viti Maalum wa Manispaa ya Musoma,Mh Sister Yohana, amewakabidhi waendesha bodaboda wa Kata ya Mwisenge eneo la Mtakuja banda maalum la kujikinga na mvua na jua wanapokuwa wakisubiri abiria.
Banda hilo limejengwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtakuja, Manispaa ya Musoma, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha vijana hao kuendelea na shughuli zao za usafirishaji bila kuathiriwa na hali ya hewa, hususan wakati wa mvua.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa banda hilo, Sister Yohana amesema ameamua kutekeleza ujenzi huo kwa kutambua umuhimu wa kuwaunga mkono vijana wanaotegemea shughuli za bodaboda kujipatia kipato na kuendesha maisha yao.
“Mimi kama Diwani wa Viti Maalum nimeamua kuwajengea kivuli vijana wa bodaboda wa Mtakuja, ambao ni majirani kabisa na nyumbani kwangu. Nimefanya hivi kwa kutambua juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwajali na kuwawezesha vijana,” amesema.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mchango wake katika kuboresha mazingira ya kazi kwa vijana hao, hasa wakati huu ambapo mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha.
“Nimeweza kufanya kwa nafasi yangu ili kuwasaidia vijana hawa kupata eneo la kujikinga na jua pamoja na mvua wanapokuwa wakitafuta riziki. Sitaki mvua zinaponyesha washindwe kuendelea na shughuli zao kwa kukosa sehemu ya kujisitiri,” amesema.
Sister Yohana amewataka waendesha bodaboda kulitunza banda hilo na kulitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, ili liweze kuwa msaada kwao kwa muda mrefu.
Nao masfisa usafirishaji maarufu kama boda boda wamemshukuru diwani huyo kwa matendo yake ya huruma ambpo wameiomba Serikali kuwapa fursa za mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kumiliki vyombo vyao vya usafiri, wakieleza kuwa bodaboda wanazochukua kwa mikataba kutoka kwa mabosi zinawaumiza kutokana na masharti magumu ya mikataba hiyo.
Wamesema mikopo ya Serikali ina masharti nafuu na riba ndogo, hivyo wamemuomba Mhe. Diwani kuwapa kipaumbele katika upatikanaji wa mikopo hiyo ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao kwa uhuru na kuongeza kipato.
Aidha, vijana hao wamemshukuru na kumpongeza Mhe. Diwani kwa hatua mbalimbali anazochukua kuwasaidia vijana, huku wakiiomba Serikali kuhakikisha fursa za mikopo zinawafikia vijana wengi zaidi, wakiwemo wale ambao majina yao hayajafika kwenye orodha za wanufaika.





Comments
Post a Comment