Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema hakuna mipango ya maendeleo ya Taifa inayoweza kufanikiwa bila mchango wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Sangu ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea banda la NBS katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Waziri huyo amesema upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati ni nguzo muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya Taifa, kwa kuwa takwimu zinazokusanywa, kuchambuliwa na kuhifadhiwa na NBS husaidia Serikali pamoja na wadau wengine kufanya maamuzi yanayozingatia uhalisia wa mahitaji ya wananchi.
Kwa mujibu wake, uwepo wa takwimu sahihi unawezesha kuweka vipaumbele vya maendeleo, kuandaa mipango na kufuatilia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Taifa.
Amesisitiza umuhimu wa NBS kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu, huku akitoa wito wa kuhakikisha taarifa hizo zinapatikana kwa wakati na kutumiwa ipasavyo.
Sangu pia amesema kazi ya NBS ina umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inalenga kuweka misingi ya maendeleo endelevu na kuongeza ustawi wa wananchi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amepongeza ushiriki wa NBS katika maonesho hayo ya kimataifa ya madini, akisema ni fursa kwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali kufahamu zaidi majukumu ya taasisi hiyo na namna takwimu zinavyoweza kutumika katika shughuli za kiuchumi na maendeleo.



Comments
Post a Comment