MWANZA.
Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika tafiti za zao la pamba, kwa lengo la kupata suluhisho za kisayansi na kiteknolojia zitakazosaidia kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Menejimenti ya TCB na TARI kilichofanyika Septemba 18, 2026 katika Ofisi za Bodi ya Pamba Tanzania, Makao Makuu jijini Mwanza.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Mhandisi Godwin Makori, amesema utafiti unapaswa kuelekezwa zaidi katika changamoto zinazowakabili wakulima, huku matokeo yake yakifikishwa kwa wakati kwa mtumiaji wa mwisho.
“Moyo wa maendeleo ya nchi ni utafiti, lakini thamani ya utafiti inaonekana pale matokeo yake yanapomfikia mtumiaji wa mwisho na kutatua changamoto aliyonayo,” amesema Mhandisi Makori.
Amesema maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika tafiti za pamba ni pamoja na afya ya udongo, mbegu, magonjwa ya mimea, mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya zana za kilimo na teknolojia zinazoweza kuongeza tija.
Mhandisi Makori pia amesisitiza umuhimu wa wataalamu wanaowahudumia wakulima kuelewa matokeo ya tafiti ili waweze kutoa ushauri sahihi na kushughulikia changamoto zinazowasilishwa na wakulima kwa wakati.
Amesema mabadiliko ya tabianchi yanaongeza umuhimu wa kufanya tafiti za mbegu zinazoweza kuhimili mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, sambamba na kubuni zana rahisi zitakazosaidia kukabiliana na changamoto ya magugu katika mashamba ya pamba.
Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuweka mfumo madhubuti wa mtiririko wa taarifa unaoanzia kwa mkulima, kufikishwa kwa watafiti na hatimaye matokeo ya utafiti kurejeshwa kwa mkulima.
Katika eneo la mbegu, Mhandisi Makori amependekeza kuimarishwa kwa ukaguzi katika hatua zote za uzalishaji na usambazaji ili kupunguza uwezekano wa kuenea kwa magonjwa ya pamba.
Pia amependekeza kufanyika kwa tafiti shirikishi za magonjwa ya pamba zitakazowahusisha wakulima na wataalamu wa utafiti, ili kupata taarifa sahihi kutoka katika maeneo ya uzalishaji.
Amesema TCB na TARI zinapaswa kuendelea kushirikiana katika kukamilisha mchakato wa usajili wa mbolea hai ya pamba inayojulikana kama Go-Biofert, wakati Bodi ikiendelea na maandalizi ya uwekezaji wa kiwanda cha kuzalisha mbolea hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, amesema taasisi hiyo itaendelea kuimarisha tafiti zenye ubunifu na zinazozingatia maendeleo ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika kilimo na kutoa majibu ya changamoto zinazowakabili wakulima.
Dkt. Bwana amewataka wadau wa kilimo na watumiaji wa matokeo ya tafiti kuwasilisha maeneo yanayohitaji utafiti zaidi, ili TARI iweze kuelekeza wataalamu na rasilimali katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Amesema TARI ina wataalamu zaidi ya 1,400 waliopo katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo iko tayari kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya kilimo katika kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinazalisha suluhisho zinazoweza kutumiwa na wakulima.
Dkt. Bwana pia ameipongeza TCB kwa ushirikiano wake na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru, hususan katika kuwezesha kifedha shughuli mbalimbali za utafiti zinazolenga kuendeleza zao la pamba.
Akizungumzia suala la mbegu, amesema kwa sasa nchini inatumika aina moja ya mbegu ya pamba kibiashara, huku aina nyingine 17 zikiwa katika hatua mbalimbali za utafiti.
Amesema TARI itafanyia kazi pendekezo la kuwa na aina zaidi ya moja za mbegu za pamba zinazoweza kutumika kibiashara kulingana na mahitaji ya wakulima na matokeo ya tafiti.
Aidha, amesema Gene Bank inayojengwa mkoani Arusha itakapokamilika itawezesha uhifadhi wa vinasaba na vizazi vya mbegu kwa muda mrefu, hatua itakayosaidia kuhifadhi rasilimali za kijenetiki za mazao.
Katika matumizi ya teknolojia, Dkt. Bwana amesema kuna umuhimu wa kutumia akili unde (AI) katika utambuzi wa magonjwa ya pamba, ikiwemo mnyauko fusari, ili kuwezesha utambuzi wa changamoto mapema na kuchukua hatua stahiki.
Katika hitimisho la kikao hicho, TCB na TARI zimekubaliana kuunda kamati ndogo ya pamoja ya wataalamu itakayoshughulikia masuala ya utafiti, ushauri wa kitaalamu kuhusu zao la pamba na ufuatiliaji wa utekelezaji wa tafiti.
Kamati hiyo pia itasaidia kuimarisha mawasiliano kati ya wakulima, Bodi, watafiti na wadau wengine, pamoja na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanafanyiwa kazi na kufikishwa kwa mkulima.
Ushirikiano huo unalenga kuongeza kasi ya upatikanaji wa suluhisho za kisayansi na kiteknolojia kwa changamoto za uzalishaji wa pamba, kuongeza tija kwa mkulima na kuchangia katika kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.




Comments
Post a Comment