Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amezindua rasmi Mashindano ya Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) 2026, katika hafla iliyofanyika tarehe 21 Septemba, 2026, katika Uwanja wa CCM Kirumba, Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Mhe. Hemed amewataka wanamichezo na washiriki wote kutumia mashindano hayo kuonesha vipaji, nidhamu na uwezo wao, huku wakizingatia misingi ya haki, sheria na maadili ya michezo.
Aidha, amewataka waamuzi na waendeshaji wa mashindano hayo kutekeleza majukumu yao kwa haki na weledi, huku wachezaji na washiriki wengine wakitakiwa kuheshimu sheria na kudumisha nidhamu wakati wote wa mashindano.
“Tusishindane kwa nguvu na kwa uwezo wetu bali tushindane kwa heshima, utu na kwa kufuata misingi ya michezo, huku tukitambua kuwa kuna maisha wakati wa michezo na maisha baada ya michezo,” amesema Mhe. Hemed.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho, wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mashindano hayo, amewataka wananchi kutumia kaulimbiu ya BAMMATA 2026 katika kuendeleza amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Mashindano hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu “BAMMATA 2026, Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kudumisha amani.”
Dkt. Nyansaho amesema kaulimbiu hiyo inawakumbusha Watanzania wajibu wao wa pamoja wa kuendelea kulinda umoja, amani na mshikamano wa Taifa, kupitia michezo na shughuli nyingine zinazowaunganisha wananchi.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda, amesema mashindano hayo ni sehemu ya juhudi za kuibua na kukuza vipaji vya wanamichezo nchini.
Amesema Jeshi limejipanga kuboresha mfumo wa utambuzi na ukuzaji wa vipaji, kuimarisha miundombinu ya michezo pamoja na kuweka mazingira bora kwa wanamichezo ili waweze kutimiza uwezo wao.
“Dhamira yetu ni kuona Vyombo vya Ulinzi na Usalama vinazidi kuwa chimbuko la vipaji bora na kuwa sehemu ya mafanikio ya Taifa letu katika medani za michezo,” amesema Jenerali Mkunda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CP Salum Hamduni, amelishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na uongozi wa BAMMATA kwa kulichagua Jiji la Mwanza kuwa mwenyeji wa mashindano hayo mwaka huu.
Mhe. Hamduni amesema ujio wa mashindano hayo jijini Mwanza utatoa fursa kwa wananchi kukuza shughuli zao za kiuchumi na biashara kutokana na ongezeko la mwingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Hafla ya ufunguzi wa Michezo ya Majeshi Tanzania, inayowakutanisha wanamichezo kutoka pande zote mbili za Muungano wa Tanzania, imehudhuriwa na viongozi wa Chama na Serikali wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Faraji Kasidi Mnyepe, wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na wakuu wa Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, hafla hiyo imehudhuriwa na maafisa na askari kutoka pande zote mbili za Muungano, pamoja na maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza waliojitokeza kushuhudia uzinduzi wa mashindano hayo.
Mashindano ya BAMMATA 2026 yanatarajiwa kuendelea kwa kushirikisha wanamichezo kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Tanzania katika michezo mbalimbali, huku yakilenga kuimarisha umoja, mshikamano, nidhamu na utamaduni wa michezo nchini.











Comments
Post a Comment