Programu ya Pili ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ II) inatarajiwa kutoa fursa kwa vijana kushiriki katika mafunzo ya ufundi na ufundi stadi na kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira. Hayo yameelezwa kwenye mafunzo ya siku tatu yaliyoanza tarehe 22 Septemba, 2026 Mjini Morogoro kwa taasisi zinazo tekeleza programu ya ESPJ II yenye lengo la kujengeana uelewa juu ya miongozo ya Urekebu wa elimu ya Ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) nchini ili kuhakikisha taasisi zinazotekeleza programu ya ESPJ II zinapata uelewa mpana kuhusu sheria, miongozo, viwango na taratibu za NACTVET zinazopaswa kuzingatiwa katika utoaji wa elimu ya Ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa NACTVET tarehe 23 Septemba, 2026, Mkurugenzi wa Udahili, Utahini na Utunuku, Dkt. Marcelina Baitilwake amesema, mafunzo hayo ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja na kuhakikisha kwamba kila taasisi nufaika inatimiza wajibu wake katika utekelezaji wa ESPJ II.
Aidha, amewataka washiriki kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo kwa kutoa maoni, kuuliza maswali, kubadilishana uzoefu na kubainisha maeneo ambayo wanaona yana changamoto ili yaweze kufanyiwa kazi.
Dkt. Bailtiwake ameeleza kuwa, Serikali imeziamini na kuzikabidhi taasisi hizo jukumu la kujenga ujuzi kwa vijana na kuchangia maendeleo ya Taifa, hivyo ni muhimu utekelezaji wa shughuli zote uzingatie sheria, miongozo na viwango vilivyowekwa ili kufikia malengo yanayotarajiwa na Serikali.
Aidha, amesisitiza ushirikiano miongoni mwa taasisi nufaika ni muhimu ili kuhakikisha kwamba malengo ya mradi yanafikiwa na manufaa yaliyokusudiwa yanawafikia walengwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya ESPJ II kutoka NACTVET Dkt. Aggrey Mleli, ameeleza kwamba, NACTVET kama mrekebu wa TVET inafanya jitihada za dhati kuhakiksha kwamba inatimiza wajibu wake katika kutekeleza program hii ikiwa ni pamoja na kutoa msaada unaohitajika kwa watekelezaji wengine kwa wakati. Aidha, amewaomba washiriki kupitia maeneo yao ya utekelezaji, kuainisha maeneo ambayo taasisi zao zinahitaji msaada wa NACTVET ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati na kuondoa vikwazo vyoyote vinavyoweza kuchelewesha kufikiwa malengo ya program hii.
Programu ya ESPJ II inalenga kuongeza fursa kwa vijana kushiriki katika mafunzo ya ufundi na ufundi stadi na kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri. Aidha, programu inalenga kuimarisha ubora na upatikanaji wa mafunzo, kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa endelevu na wenye manufaa kwa walengwa, na hatimaye kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa.
Utekelezaji wa Programu ya ESPJ II unahusisha Wizara, Taasisi mbalimbali ikiwemo NACTVET pamoja na taasisi za elimu na mafunzo.




Comments
Post a Comment