Na Wellu Mtaki, Geita
Benki ya Azania imeweka mkakati wa kuimarisha na kuongeza tija katika sekta ya madini nchini kwa kuwawezesha wadau mbalimbali wa sekta hiyo kupata mikopo yenye masharti rafiki, inayolenga kukidhi mahitaji ya kifedha katika hatua tofauti za mnyororo wa thamani wa madini, kuanzia wachimbaji wadogo hadi wawekezaji wakubwa.
Kwa mujibu wa benki hiyo inayoshiriki Maonesho ya Tisa ya Madini Geita, imeeleza kuwa inatoa mikopo ya mitaji inayolipwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu kwa ajili ya kuendesha na kukuza biashara.
Aidha, benki hiyo imeeleza kuwa inawezesha wadau wa sekta ya madini kupata mikopo kwa ajili ya ununuzi wa vyombo vya usafirishaji, ikiwemo magari, malori na matipa, ambavyo ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa vifaa na mazao ya madini kutoka eneo moja kwenda jingine.
Kwa upande wa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu, Benki ya Azania imekuja na bidhaa maalumu kwa wateja wanaouza dhahabu yao kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kupitia huduma hiyo, benki inaweza kutoa mkopo wa hadi Shilingi bilioni 5 bila dhamana, hatua inayolenga kuwawezesha wachimbaji kuendelea na shughuli zao bila kusubiri malipo yao kukamilika.
Sharti la msingi kwa mteja anayehitaji huduma hiyo ni kutumia akaunti ya Azania, ambapo benki inaweza kumpatia hadi asilimia 80 ya fedha anazotarajia kupokea kutoka BoT. Mfumo huo unamwezesha mteja kupata mtaji wa kuendeleza shughuli zake wakati akisubiri mchakato wa malipo kukamilika.
Katika hatua nyingine ya kusaidia maendeleo ya vijiji vinavyozunguka maeneo ya migodi, Benki ya Azania imetangaza makubaliano na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Makubaliano hayo yanalenga kuwawezesha wajasiriamali kujenga vituo na maeneo ya huduma za mafuta vijijini kwa kupata mikopo yenye riba nafuu ya asilimia tano kwa mwaka.
Kwa mujibu wa benki hiyo, mpango huo unalenga kuongeza upatikanaji wa nishati katika maeneo ya vijijini na kuchochea shughuli za uzalishaji, biashara na huduma zinazohusiana na sekta ya madini pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi.
Kwa wawekezaji wenye mipango ya muda mrefu, Benki ya Azania inatoa mikopo ya uwekezaji ya hadi miaka nane kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, magari na mahitaji mengine muhimu yatakayowawezesha kuongeza uzalishaji, ufanisi na uwezo wa kufanya shughuli za uchimbaji kwa kiwango kikubwa zaidi.


Comments
Post a Comment