Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Bagamoyo, Joseph Bureta, ameipongeza shule ya msingi na awali ya Twibhoki kwa kuendelea kufaulisha vyema wanafunzi katika masomo ya sayansi
Bureta amesema hayo leo Septemba 19, 2026 katika mahafali ya nne ya wanafunzi 14 wa Shule ya Msingi na Awali ya Twibhoki, iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo amewataka wahitimu kutumia ipasavyo elimu waliyoipata na kujiepusha na marafiki wenye tabia zinazoweza kukatisha ndoto zao za kielimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Issa Juma Kiango, amewataka wazazi wa wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa shule kwa kuthamini elimu bora waliyoipata watoto wao na kuendeleza ushirikiano na uongozi wa shule.
Naye Mkuu wa Shule ya Twibhoki, Peter Chacha, amempongeza Mkurugenzi wa shule hiyo, Grace Warioba, kwa kuendelea kutoa mchango katika maendeleo ya shule hiyo, huku akiwataka wahitimu kuwa wavumilivu na kukabiliana kwa ujasiri na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika safari yao ya elimu.
Chacha amesema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma na kufanikiwa kupata ufaulu mzuri wa daraja A, akieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya uongozi wa shule, kamati ya shule, walimu, wazazi, wadau wa elimu pamoja na Serikali ya Tanzania.
Aidha, Mwalimu wa Masomo ya Sayansi shuleni hapo, Sadiki Ezekiel, amewataka wazazi kuwahamasisha watoto wao kupenda masomo ya sayansi, akisema taaluma hizo zina umuhimu mkubwa katika kukidhi mahitaji ya sasa ya teknolojia na maendeleo ya huduma za kisayansi nchini.
Kwa upande mwingine, mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Kassim amewahimiza wazazi kuchagua Shule ya Twibhoki kwa ajili ya watoto wao, akieleza kuwa shule hiyo ina miundombinu bora na mazingira rafiki ya ufundishaji na ujifunzaji yanayochangia kuboresha maendeleo ya wanafunzi.
Naye mwanafunzi wa shule hiyo, John Joel, amewataka wanafunzi wenzake kuweka bidii katika masomo na kupenda kujifunza, hususan masomo ya sayansi, ili waweze kufikia ndoto na malengo waliyojiwekea katika maisha yao.



















Comments
Post a Comment