MBUNGE wa Jimbo la Serengeti, Mhe. Mary Daniel Surati (MB), amepata heshima kubwa baada ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa washiriki 40 wa kundi la kwanza la waanzilishi (Founding Fellows) wa programu ya African Academy for Women in Political Leadership, inayotekelezwa kupitia African School of Governance (ASG).
Uteuzi huo umefanyika baada ya mchakato wa ushindani uliowashirikisha waombaji 1,334 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, jambo linaloonyesha kiwango cha juu cha ushindani na ubora wa washiriki waliochaguliwa kujiunga na programu hiyo ya kimataifa inayolenga kuwaandaa wanawake viongozi wa kizazi kipya barani Afrika.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mhe. Surati amesema anajivunia kuwa sehemu ya kundi la kwanza la waanzilishi wa programu hiyo, akieleza kuwa ni fursa muhimu ya kujifunza, kukuza uwezo wake wa uongozi na kujenga mtandao wa ushirikiano na wanawake viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Amesema mafunzo hayo yatamwezesha kupata maarifa mapya kuhusu uongozi wa kisiasa, utawala bora, utungaji wa sera na mbinu za kushughulikia changamoto za maendeleo, huku yakimpa nafasi ya kubadilishana uzoefu na viongozi wengine wenye maono ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.
"Programu hii itanijengea uwezo mkubwa wa kiuongozi na kunipa fursa ya kujifunza pamoja na kushirikiana na viongozi wenzangu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, ili niendelee kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Serengeti na Watanzania kwa ufanisi, ubunifu na uzalendo zaidi," amesema Mhe. Surati.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwakutanisha wanawake viongozi kutoka sekta mbalimbali barani Afrika kwa lengo la kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kisiasa, kuendeleza utawala bora na kuchochea maendeleo jumuishi katika nchi zao.
Mbali na kuwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mhe. Mary Daniel Surati pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara na Mwanzilishi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Nyayo Tanzania, ambapo ameendelea kujihusisha na shughuli mbalimbali za maendeleo na uwezeshaji wa jamii, hususan vijana na wanawake.

Comments
Post a Comment