Na Wellu Mtaki, Geita
WACHIMBAJI wa madini washauriwa kutumia huduma za maabara na vipimo vya kisayansi kubaini aina na kiwango cha madini katika sampuli zao kabla ya kuingia katika gharama kubwa za uchimbaji na uchenjuaji.
Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, John Faustine, amesema matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchunguzi wa sampuli yanaweza kumsaidia mchimbaji kufanya maamuzi sahihi na kuepuka hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu madini yaliyopo.
Faustine amesema maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali zina vifaa vya kisasa vinavyowezesha uchunguzi wa sampuli za madini na kubaini uwepo wa madini mbalimbali kulingana na mahitaji ya mdau.
Amesema huduma hiyo ni muhimu kwa wachimbaji kwa sababu baadhi ya sampuli zinaweza kuwa na madini mengine yanayoweza kuathiri mchakato wa uchenjuaji, hivyo taarifa za kisayansi huwasaidia wachimbaji kupanga njia sahihi ya kuchakata madini yao.
“Kwa mfano, kwenye dhahabu kunaweza kuwepo madini shindani ambayo yanaweza kuongeza gharama wakati wa uchenjuaji. Kupitia uchunguzi wa kimaabara, mdau anaweza kubaini uwepo wa madini hayo na kuchukua tahadhari mapema,” amesema Faustine.
Aidha mesema Mamlaka hiyo inalenga kuhakikisha wachimbaji wanapata majibu sahihi kwa wakati ili waweze kufanya maamuzi ya kitaalamu badala ya kutegemea makadirio yasiyo na uhakika.
Faustine amesema pamoja na uchunguzi wa madini, Mkemia Mkuu wa Serikali ana jukumu la kusimamia matumizi ya kemikali za viwandani na majumbani, ikiwemo katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Amesema mamlaka hiyo husajili kemikali, wadau wanaojihusisha na matumizi yake pamoja na maeneo ambayo kemikali hizo zinatumika.
Aidha, amesema Mkemia Mkuu wa Serikali hufanya ukaguzi na kutoa elimu kwa watumiaji wa kemikali kuhusu matumizi sahihi na salama, kwa lengo la kulinda afya za watumiaji, jamii pamoja na mazingira.
“Teknolojia ya uchimbaji wa madini inahusisha matumizi ya kemikali kwa kiwango kikubwa, hivyo ni muhimu kuhakikisha zinatumika kwa usalama ili kulinda mtumiaji, jamii na mazingira,” amesema.
Kwa upande mwingine, Faustine amesema Mkemia Mkuu wa Serikali ana mamlaka ya kusajili maabara zinazofanya vipimo vya kemikali na sayansi ili kuhakikisha zinatoa huduma kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wadau wanapata majibu sahihi na kwa wakati, kwani majibu yasiyo sahihi yanaweza kumfanya mtumiaji kufanya uamuzi usio sahihi na kuingia katika hasara.
Ameongeza kuwa maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali pia hufanya uchunguzi wa ubora wa bidhaa na mazingira, pamoja na uchunguzi wa uwepo wa madini mbalimbali kulingana na mahitaji ya wadau.
Faustine amesema Mkemia Mkuu wa Serikali pia hushirikiana na wadau wa tiba asili na tiba mbadala katika kuhakikisha bidhaa zinazotokana na mimea na vyanzo vingine vya asili zinakuwa salama na zenye ubora.
Amesema wataalamu wa maabara hufanya uchunguzi wa bidhaa hizo kwa kuangalia ubora, usalama na uwepo wa viambata vinavyohusishwa na dawa husika.
Baada ya kupata majibu ya vipimo, amesema wazalishaji na wasindikaji wa dawa asili wanaweza kutumia taarifa hizo katika taratibu za usajili kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Faustine amesisitiza umuhimu wa wadau kutumia huduma za kitaalamu na vipimo vya kisayansi ili kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi yenye tija katika shughuli zao.

Comments
Post a Comment