*MWANZA:*
Uwekezaji wa Serikali kupitia programu ya BOOST wenye thamani ya shilingi bilioni 4.2 katika kuboresha miundombinu ya elimu umeanza kuonesha matokeo chanya, baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kushika nafasi ya tatu kimkoa katika matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2026.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Dkt. Festo Ndugange, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo, ambapo alikutana na walimu, wanafunzi, wazazi, viongozi na wananchi, baada ya kukagua ujenzi wa Shule mpya ya Awali na Msingi ya Isamilo.
Mradi huo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 540.3 unahusisha ujenzi wa vyumba 14 vya madarasa, jengo moja la utawala, matundu ya vyoo pamoja na upatikanaji wa samani za shule.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Ndugange amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu kuanzia mwaka 2021 hadi 2026, kwa kujenga miundombinu na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kuboresha mazingira ya elimu, akieleza kuwa miundombinu iliyojengwa inatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza katika mazingira bora na yenye kuvutia.
Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa matokeo mazuri ya kitaaluma, huku akiwataka wazazi kuendelea kuwapeleka watoto shule na kushirikiana na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Pia, amesisitiza umuhimu wa viongozi, walimu, wazazi na wanafunzi kutunza miundombinu pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia vilivyowekezwa na Serikali ili vidumu na kuendelea kutoa huduma kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Fatuma Mganga, amesema uwekezaji kupitia programu ya BOOST umeleta matokeo chanya katika sekta ya elimu, hususan wilayani Sengerema, akiwataka viongozi kuendelea kusimamia na kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Nganga, ameishukuru Serikali kwa fedha zilizotolewa kutekeleza miradi ya maendeleo, akiahidi kuwa viongozi wa wilaya hiyo wataendelea kusimamia miradi yote, ikiwemo ya BOOST, ili wananchi wanufaike na huduma bora na kuinuka kiuchumi na kijamii.













Comments
Post a Comment