Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Agness Marwa, amekabidhi matofali 1,000 na mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio unaozunguka wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Nyasho, Manispaa ya Musoma, hatua inayolenga kulinda faragha za mama wajawazito wakati wa kupata huduma za uzazi.
Akizungumza wakati wa kutembelea kituo hicho, Mhe. Agnes Marwa amesema ameamua kutoa mchango huo kwa hiari yake baada ya kubaini changamoto inayowakabili kinamama wanaojifungua, akisisitiza kuwa hataki kusubiri wananchi wamfuate kumuomba msaada, bali ana wajibu wa kufuatilia na kutambua mahitaji yao mwenyewe.
Pia amekishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwapa wabunge nafasi pana ya kutekeleza majukumu yao, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwataka wabunge kutoka na kuwafuata wananchi ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Mhe. Marwa amesema kama ilivyo kwa jukumu la malezi, yeye kama mama ana wajibu wa kufahamu changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wanawake na watoto, na kuchukua hatua pale anapoona kuna uhitaji.
“Nimejileta mwenyewe, bila kuagizwa wala kuombwa na mtu yeyote. Nimeleta hapa matofali 1,000 na mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya ujenzi,” amesema Marwa.
Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyasho, Dkt. Richard Majahasi, amesema kituo hicho kinapakana na barabara, hali inayosababisha wagonjwa kuonekana na watu wanaopita, hususan mama wajawazito wanaopata huduma katika wodi ya wazazi.
Amesema nyakati za usiku, kutokana na joto ndani ya vyumba, wauguzi hulazimika kufungua mapazia ili kuruhusu hewa kuingia, lakini hali hiyo inasababisha wagonjwa kuonekana hadi ndani ya vyumba kutokana na kutokuwepo kwa uzio wa kutosha.
Ameeleza kuwa changamoto hiyo inaathiri faragha za wanawake wakati wa kujifungua, huku kituo hicho kikihudumia wastani wa wanawake 200 hadi 300 kwa mwezi, jambo linaloonesha umuhimu wa kuwa na uzio imara utakaolinda usiri wao.
Aidha, Dkt. Majahasi ameishukuru Ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa pamoja na Serikali ya Mtaa kwa kuendelea kusaidia kuboresha kituo hicho, ikiwemo uboreshaji wa vyumba vitatu vya kujifungulia kwa kuweka sehemu za kutenganisha wagonjwa ili kuongeza faragha.
Hata hivyo, amesema bado kuna mahitaji ya maboresho zaidi, ikiwemo ujenzi wa uzio utakaowezesha wanawake kupata huduma za uzazi katika mazingira salama na yenye heshima.
Mchango huo wa Mbunge Agness Marwa unatarajiwa kusaidia kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya ya uzazi katika Kituo cha Afya Nyasho, kwa kuhakikisha mama wajawazito wanapata huduma muhimu huku faragha na heshima yao vikilindwa.









Comments
Post a Comment