SENGEREMA, MWANZA
Kamati ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza, imefanya kikao cha maandalizi ya kuweka na kupitisha mpango kazi wa utekelezaji wa mradi wa Safe Future Mtoto Initiative.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Afisa Mradi wa Safe Future Mtoto Initiative, Scholastica Misana, amesema Shirika la SOS Children's Villages Tanzania kupitia mradi huo limepanga kutekeleza shughuli mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo wanawake na vijana wa rika balehe katika kujitegemea kiuchumi, kutoa elimu ya afya pamoja na kuwajengea uwezo wa kujikinga na kuepuka vitendo vya ukatili.
Aidha, amesema mradi huo unalenga kuimarisha mifumo ya Serikali kwa kutumia teknolojia za kidijitali ili kuongeza ufanisi katika kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Ameeleza kuwa mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika mikoa miwili ya Mwanza na Dar es Salaam, kupitia halmashauri nne ambazo ni Ilemela, Magu, Sengerema na Temeke.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Wakili Agape Fue, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya MTAKUWWA, amewataka wajumbe na wataalamu kuhakikisha wanajiandaa ipasavyo katika kutekeleza malengo na mpango kazi utakaowekwa.
Amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mpango huo kuzingatia miongozo, kanuni na sheria zilizopo ili kuhakikisha wanawake na watoto wanapata ulinzi, haki na mazingira bora ya kuishi na kustawi.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Nyanjige Julius, ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo utazingatia maeneo nane muhimu pamoja na majukumu ya Kamati ya MTAKUWWA katika kuratibu juhudi za kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia sekta na wadau mbalimbali wa jamii.
Sambamba na maandalizi hayo, mradi huo unaendelea kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali katika jamii, yakiwemo wauguzi, watoa huduma za afya ngazi ya jamii, wazee maarufu na makundi mengine.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kutambua viashiria vya ukatili, kuhamasisha jamii kuchukua hatua na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili vinavyotokea majumbani, katika taasisi za elimu kama shule na vyuo, pamoja na maeneo mengine ya jamii.












Comments
Post a Comment