Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imeendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya kemikali nchini kwa kufanya usajili, ukaguzi na kutoa elimu ya matumizi salama ya kemikali kwa kulinda afya za wananchi na mazingira.
Akizungumza Leo Septemba 30, 2026 Katika maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Katika Viwanja vya Dkt. Samiaa Suluhu Hassan Mkoani Geita
Faustine amesema mamlaka hiyo inasimamia sheria tatu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo sheria inayohusu usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani.
Amesema Mkemia Mkuu wa Serikali ndiye msajili wa kemikali zote nchini, ambapo anasajili wadau, kemikali pamoja na maeneo yanayotumika kemikali hizo, ikiwemo katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Kwa mujibu wa meneja huyo, GCLA pia hufanya ukaguzi na kutoa elimu kwa watumiaji wa kemikali kuhusu matumizi sahihi na salama ili kupunguza madhara kwa afya, jamii na mazingira.
Amesema mamlaka hiyo ina maabara zenye ithibati na mitambo ya kisasa inayotumika kuchunguza madini na bidhaa, pamoja na kusaidia wachimbaji kubaini uwepo na ubora wa madini.
Ameongeza kuwa maabara hizo husaidia pia kutambua madini shindani yanayoweza kujitokeza wakati wa uchenjuaji wa dhahabu, hatua inayowawezesha wadau kuchukua tahadhari au kutumia njia mbadala ili kuepuka hasara.
Aidha, GCLA ina jukumu la kusajili maabara za kemikali na sayansi jinai ili kuhakikisha zinatoa majibu sahihi na ya kuaminika kwa wakati.
Katika tiba asili na tiba mbadala, amesema GCLA hushirikiana na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kupima usalama, ubora na viambata sumu katika dawa zinazotengenezwa kwa kutumia mimea, pamoja na kutoa elimu ya usindikaji bora ili bidhaa hizo zikidhi viwango na kuwa na ushindani sokoni.
Kuhusu zebaki, amesema Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Minamata unaolenga kusitisha matumizi ya zebaki ifikapo mwaka 2030 kutokana na madhara yake, huku GCLA ikiendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya kemikali mbadala katika uchenjuaji wa madini.


Comments
Post a Comment