MBUNGE wa Jimbo la Musoma Mjini na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Mgore Miraji Kigera, ni miongoni mwa viongozi wanaoshiriki ziara ya kikazi nchini Italia yenye lengo la kujifunza teknolojia na mifumo ya uzalishaji wa vifaa vya reli, ili kutathmini uwezekano wa Tanzania kuanzisha kiwanda cha ndani kitakachopunguza gharama za uendeshaji na kuimarisha ufanisi wa huduma za usafiri wa reli.
Ziara hiyo inalenga kupata uzoefu wa teknolojia ya kisasa katika uzalishaji wa reli, mifumo ya kubadilishia njia za treni (Switches), vipuri na vifaa vingine muhimu vinavyotumika katika ujenzi, matengenezo na uendeshaji wa miundombinu ya reli.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kigera ameungana na ujumbe wa Kamati kutembelea kiwanda cha RFI (Rete Ferroviaria Italiana), kilichopo Pontassieve nchini Italia, kinachojihusisha na utengenezaji wa vifaa na mifumo mbalimbali inayotumika katika sekta ya reli.
Kupitia ziara hiyo, imelenga kujifunza mifumo ya uzalishaji na uendeshaji wa kiwanda hicho ili kupata maarifa yatakayosaidia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutathmini uwezekano wa kuanzisha kiwanda cha aina hiyo nchini, hatua itakayopunguza utegemezi wa vifaa kutoka nje ya nchi na gharama zinazotokana na uagizaji wake.
Uwekezaji huo ukitekelezwa utasaidia kuongeza upatikanaji wa vifaa kwa wakati, kupunguza ucheleweshaji wa matengenezo na kuimarisha uwezo wa TRC kutoa huduma za usafiri wa reli kwa ufanisi zaidi, sambamba na kukuza uzalishaji wa viwanda vya ndani.
Ziara hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Suleiman Kakoso, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Eng. Machibya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji nchini.
Katika ziara hiyo, pia Spika wa Bunge, Katibu wa Bunge, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mkurugenzi wa Miundombinu wa Wizara ya Uchukuzi pamoja na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Reli Tanzania wameambatana Kwa dhamira Moja ya kufanikisha sekta ya usafiri na usafirishaji nchini.


Comments
Post a Comment