Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Ndg. Mary Pius Chatanda (MCC), amewapongeza na kuwashukuru wanawake wa Pemba kwa mchango wao katika kutekeleza Mpango Mkakati wa UWT, uliolenga kuhamasisha ushiriki wa wanachama na kuimarisha maandalizi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza Novemba 19, 2026, katika mkutano wa ndani na wanawake pamoja na wanachama wa CCM Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, Chatanda amesema ushiriki na kujituma kwa wanawake hao katika kutekeleza mpango huo ulikuwa sehemu ya juhudi za pamoja zilizochangia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2025, ambapo CCM ilipata ushindi.
Amesema wanawake wameendelea kuwa sehemu muhimu katika shughuli za Chama, hivyo amewataka kudumisha mshikamano, umoja na ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya UWT na kuendeleza shughuli za CCM katika maeneo yao.
Aidha, Chatanda amewahimiza wanachama wa CCM kuendelea kuhamasishana kuhusu usajili wa wanachama wapya pamoja na kulipia ada za uanachama kwa njia ya kielektroniki, akieleza kuwa matumizi ya mfumo huo yanalenga kurahisisha michakato ya uanachama, kuongeza ushiriki na kupanua wigo wa wanachama wa Chama.
Ameongeza kuwa ni muhimu kila mwanachama kutambua wajibu wake katika kuimarisha taasisi za Chama kupitia ushiriki wake katika shughuli mbalimbali, hatua itakayosaidia kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama.





Comments
Post a Comment