Na Mwanamkuu Mwandoro, Tanga.
SEKTA ya madini mkoani Tanga imeendelea kuimarisha mchango wake katika uchumi wa mkoa na taifa, huku uwekezaji mpya ukitarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, ajira na fursa za biashara kwa wananchi.
Afisa Madini wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Laurent Bujashi, amesema katika mwaka wa fedha uliopita mkoa ulikusanya Sh13.9 bilioni kupitia tozo na maduhuli yanayosimamiwa na mamlaka za madini, kiasi kilichovuka lengo la Sh11 bilioni kwa asilimia 27.4.
Amesema makusanyo hayo yalifikia asilimia 127.4 ya lengo, bila kujumuisha kodi zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Ukiunganisha makusanyo haya na kodi zinazokusanywa na TRA, mchango wa sekta ya madini katika mapato ya Mkoa wa Tanga ni mkubwa,” amesema Bujashi
Ameeleza kuwa mchango huo unatarajiwa kuongezeka kadiri shughuli za uchimbaji zinavyopanuka na miradi mipya ya uwekezaji inavyoanza kufanya kazi.
Sambamba na hayo pia amesema Mbali na mapato ya Serikali na ajira, kampuni za madini zinatakiwa kuchangia maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo yao ya uwekezaji kupitia programu za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Mhandisi Bujashi amesema kampuni hizo zinapaswa kuwasilisha mipango ya CSR kwa mamlaka za serikali za mitaa kila mwezi Oktoba ili kujadiliwa na kupitishwa na kamati za CSR zilizoanzishwa katika halmashauri husika.
Pia zinatakiwa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo ili kuwezesha mamlaka kufuatilia iwapo ahadi zilizotolewa kwa wananchi zinatekelezwa.
Akitolea mfano, amesema Kijiji cha Stahabu, Wilaya ya Pangani, ni miongoni mwa maeneo yaliyonufaika na uwekezaji huo baada ya kupatiwa mradi wa shule wenye thamani ya Sh900 milioni kupitia Mradi wa Madini wa Tajiri unaohusishwa na kampuni ya Nyati Mineral Sands.
Amesema shule hiyo inajumuisha elimu ya awali, msingi na sekondari yenye bweni.
Maeneo mengine yaliyonufaika na miradi ya CSR inayotokana na shughuli za madini ni Kalalani, Kigwasi na Kwamsisi.
Amesema mipango hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya uchimbaji wanapata sehemu ya manufaa yatokanayo na rasilimali za madini.
Bugashi amesema Tanga ina uwezo mkubwa wa kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kati ya madini iliyopangwa kuanzishwa mkoani humo.
Ametaja kiwanda kipya cha uchenjuaji madini kinachojengwa eneo la Bosha kuwa miongoni mwa uwekezaji ambao tayari umeanza kufungua fursa kwa wakazi wa maeneo yanayokizunguka.
Amesema mradi huo umeanza kutoa ajira kwa wananchi, huku ukiibua fursa za biashara kwa watu wanaotoa bidhaa na huduma kwa wafanyakazi na wadau wengine wanaohusika na utekelezaji wake.
Pia, amesema uwekezaji huo umechangia kupanda kwa thamani ya ardhi katika maeneo yanayouzunguka, hali inayoashiria kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na mahitaji ya viwanja.
Mradi mwingine wenye matarajio makubwa ni uchimbaji wa dhahabu wa Magambasi, Wilaya ya Handeni, ambao kwa mujibu wa Bw Bugashi umeanza tena kufanya kazi licha ya kuwepo kwa migogoro ya awali kati ya kampuni zinazohusishwa na mgodi huo.
Amesema juhudi za kutatua migogoro iliyokuwepo zinaendelea sambamba na shughuli za mradi huo.
Ameendelea kusema kuwa utekelezaji wa miradi iliyopangwa, kuboreshwa kwa huduma katika sekta ya madini na kuongezeka kwa shughuli za uchenjuaji vitasaidia kuongeza thamani ya sekta hiyo katika uchumi wa Tanga.
“Mkoa una uwezo mkubwa wa kuongeza mapato yake na mchango katika uchumi wa taifa kupitia sekta ya madini. Miradi iliyopangwa ikitekelezwa kwa ufanisi, itafungua fursa zaidi kwa vijana na wananchi wengine,” amesema.
Akizungumzia mafunzo ya madini yenye lengo la kuandaa nguvu kazi itakayokidhi mahitaji ya sekta hiyo inayokua, Mhandisi Bujashi amesema Idara ya Madini imekuwa ikitoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo moja kwa moja katika maeneo yao ya kazi, hususan wakati wa ziara za ukaguzi.
Mhandisi Bujashi amesema mafunzo hayo yanalenga kuboresha mbinu za uchimbaji na kuwapatia wachimbaji ujuzi utakaowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Amesema vijana wanaotaka kujenga taaluma katika sekta ya madini wanaweza kujiunga na taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo ya ngazi ya cheti, stashahada na shahada.
Baadhi ya taasisi hizo ni Kituo cha Tanzania cha Elimu ya Vito (Tanzania Gemological Centre) kilichopo Arusha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na vyuo mbalimbali vya ufundi chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Amesema upatikanaji wa ujuzi na utaalamu unaohitajika utakuwa muhimu katika kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa shughuli za madini, ikiwemo uchimbaji, uchenjuaji na utoaji wa huduma za kitaalamu.





Comments
Post a Comment