JESHI la Polisi limeendelea kuimarisha uhusiano na vijana kupitia programu za elimu na mawasiliano, likiwataka kuwa wazalendo, kuzingatia sheria na kushiriki kikamilifu katika kulinda amani na usalama wa taifa.
Wito huo umetolewa na Afisa Polisi Jamii Mtumba, ASP Charles Mwamtobe, alipokutana na kufanya mazungumzo ya kielimu na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), Hombolo, jijini Dodoma, kupitia programu za “ONGEA NA FRESHERS” na “ONGEA NA KAMANDA.”
Katika mazungumzo hayo, vijana wamehimizwa kutambua nafasi yao katika maendeleo ya taifa kwa kuzingatia uzalendo, kuheshimu Katiba na sheria, kulinda tunu za taifa na kuepuka makundi na mienendo inayoweza kuhatarisha maisha yao na kutatiza ndoto zao.
Aidha, wamepewa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, wakitakiwa kuwa waangalifu na taarifa wanazozisambaza, kuepuka uchochezi na taarifa za uongo, pamoja na kutumia teknolojia kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.
ASP Mwamtobe pia amesisitiza umuhimu wa vijana kuwa sehemu ya kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, akibainisha kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila usalama na utulivu.
Mkutano huo pia umekuwa fursa kwa wanafunzi kueleza kero, changamoto na maoni yao kuhusu huduma za Jeshi la Polisi, hatua iliyolenga kuimarisha mawasiliano, kujenga uaminifu na kukuza ushirikiano kati ya Jeshi hilo na wananchi.
Kupitia programu hizo, Jeshi la Polisi linaendelea kuwafikia vijana katika vyuo na taasisi za elimu, likilenga kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na kuwahamasisha kuwa mabalozi wa amani katika jamii.
Vijana ni nguvu ya taifa na sehemu ya suluhisho la changamoto za leo. Uzalendo, uwajibikaji na maamuzi sahihi ya kila mmoja ni msingi wa Tanzania yenye amani, usalama na maendeleo.








Comments
Post a Comment