WANANCHI wa Kata ya Hombolo jijini Dodoma wameeleza matumaini makubwa kuhusu ujenzi wa Hombolo Thematic City, wakitarajia mradi huo kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa ajira, upanuzi wa biashara na uboreshaji wa huduma za kijamii.
Wananchi hao wamesema ujio wa mji huo wa kisasa unafungua ukurasa mpya wa maendeleo kwa wakazi wa Hombolo, huku wakisisitiza umuhimu wa kushirikishwa ili wanufaike na fursa zitakazotokana na uwekezaji huo.
Mmoja wa wananchi hao, Ndugu Magawa ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji Cha Mkoyo hombolo, amesema matarajio yao ni kuona vijana wakipata ajira na wafanyabiashara wadogo wakipanua shughuli zao, sambamba na kuimarika kwa uchumi wa eneo hilo.
Matarajio hayo yanafuatia Halmashauri ya Jiji la Dodoma kusaini mkataba na kampuni ya kimataifa ya Heerim Architecture & Planning kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Hombolo Thematic City.
Akishuhudia utiaji saini wa mkataba huo Novemba 9, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyemule, ameitaka Halmashauri ya Jiji kujiandaa kikamilifu na kuhakikisha mradi huo unasimamiwa vizuri ili utekelezwe kwa wakati.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko, amesema mradi huo unatarajia kushirikisha sekta binafsi kwa asilimia 70 ili kuharakisha uwekezaji na ujenzi wa mji huo.
Naye Msimamizi wa Mradi, William Azori, ameeleza kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ni hatua muhimu katika kuweka msingi wa utekelezaji, huku Mwenyekiti wa Heerim Architecture & Planning, Young-in Jung, akisema kampuni hiyo imejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa ufanisi na ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa.
Hombolo Thematic City ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza Dodoma kuwa jiji la kisasa linaloendana na hadhi ya Makao Makuu ya Nchi, kwa kupanua uwekezaji na kuboresha miundombinu na huduma za kijamii.
Mradi huo unakuja siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzindua Mji wa Serikali Mtumba, hatua inayokwenda sambamba na juhudi za kuimarisha hadhi ya Dodoma. Kwa wakazi wa Hombolo, matarajio ni kuona mipango hiyo ikigeuka kuwa ajira, biashara na maendeleo yenye manufaa kwa jamii.






Comments
Post a Comment