Na Mwanamkuu Mwandoro, Tanga
Kikao cha Timu ya Menejimeti ya Halmashauri ya Jiji la Tanga(CMT), kilichokaa leo, Jumatatu, Novemba 9, 2026, chini ya Mwenyekiti wake, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Bw. Philemon Mwita Magesa, kimeagiza kutolewa ilani ya siku 14 kwa wananchi wote wenye viwanja vyenye nyumba, maboma au msingi katika eneo la Kange Kasera, lakini hawajalipa malipo ya utwaaji ardhi, au wamelipa sehemu ya malipo hayo, na ambao hawatalipa kwa muda uliotolewa, wafikishwe mahakamani.
Kikao pia kimeielekeza Idara ya Maendeleo ya Ardhi na Mipango Miji, kuanza taratibu za kuviuza viwanja ambavyo havijaendelezwa (vitupu), ambapo mauzo hayo yatafanyika kupitia mfumo wa TAUSI, unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI kwa ajili ya kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri na utolewaji wa huduma mbalimbali za Serikali za Mitaa nchini Tanzania. Katika eneo hilo, kati ya viwanja 562 vilivyopimwa, viwanja 115 havijafanyiwa malipo.
Aidha CMT imeelekeza kutangazwa kwa zabuni za uondoshaji taka kwa kila kata, kuanzia na kata 12, kwa lengo la kupata wazabuni wa uondoshaji taka kwa kata ili kuboresha kazi ya udhibiti taka mjini.
Aidha Halmashauri inakusudia kufanya matengenezo na maboresho ya stendi ya mabasi ya Pongwe, Mbaraka stendi, ili iweze kutoa huduma katika mazingira bora.



Comments
Post a Comment