MKUU wa Mkoa wa Mara, Mhe. Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, amekitaka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mkoa katika kuboresha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi, akieleza kuwa hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa zimeanza kuleta matokeo chanya
Mhe. Mtambi ameyasema hayo leo Novemba 9, 2026, wakati akipokea na kufanya mazungumzo na viongozi wa CWT waliopo mkoani Mara kikazi, ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na chama hicho katika kuimarisha sekta ya elimu.
Amesema juhudi za kuboresha elimu mkoani humo zimeanza kuonesha mafanikio, akibainisha kuwa wastani wa ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba umeongezeka kutoka asilimia 66.51 mwaka 2025 hadi asilimia 73.68 mwaka 2026.
Ameeleza kuwa pamoja na Mkoa wa Mara kushika nafasi ya mwisho kitaifa katika matokeo hayo, ongezeko la ufaulu lililopatikana ni hatua muhimu inayopaswa kuendelezwa ili kuhakikisha mkoa unafanya vizuri zaidi katika matokeo yajayo.
Aidha, amesema ongezeko hilo la ufaulu limekuwa kubwa ikilinganishwa na wastani wa ongezeko la ufaulu kitaifa, jambo linaloonesha kuwa hatua zinazochukuliwa na mkoa zinaanza kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Kutokana na mafanikio hayo, Mhe. Mtambi ameitaka CWT kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kushiriki kikamilifu katika kikao cha tathmini ya elimu kinachotarajiwa kufanyika Desemba 2026.
Amesisitiza kuwa kwa kuendelea kuunganisha nguvu na wadau wa elimu, anaamini Mkoa wa Mara utaimarisha zaidi kiwango cha ufaulu katika mitihani ya kitaifa ya darasa la saba, kidato cha pili na kidato cha nne mwaka ujao.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Mwalimu Magesa Protas, amemshukuru Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wengine wa mkoa huo kwa ushirikiano wanaoutoa kwa chama hicho na walimu katika kutekeleza majukumu yao.
Amesema viongozi hao wa CWT wapo mkoani Mara kusimamia mafunzo kwa walimu wenye ulemavu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, yanayotolewa na chama hicho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika Ofisi za CWT Mkoa wa Mara.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha walimu wenye ulemavu kuimarisha uwezo wao kitaaluma na kutekeleza majukumu ya ufundishaji kwa ufanisi zaidi.




Comments
Post a Comment