UJENZI wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 89.02 kwa upande wa miundombinu, huku ujenzi wa majengo ukifikia asilimia 78.37 na ukitarajiwa kukamilika mwishoni mwa Disemba mwaka huu.
Akizungumza leo Septemba 24, 2026 katika eneo la mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa miundombinu unatarajiwa kukamilika Novemba 27, 2026, huku kazi za majengo zikikamilika Desemba 30, 2026.
Amesema katika Package ya Kwanza inayohusu miundombinu, ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege umefikia asilimia 98, njia za viungio (taxiways) asilimia 99 na eneo la maegesho ya ndege (apron) asilimia 99.
Amesema kazi nyingine zilizofikia hatua mbalimbali ni pamoja na barabara ya kuingia kiwanjani, barabara za ndani na maegesho ya magari kwa asilimia 75, mfumo wa maji asilimia 89, uzio na mageti asilimia 76, pamoja na mifumo ya umeme na vifaa vya kuongozea ndege kwa asilimia 90.
Kwa upande wa sehemu ya Pili inayohusu majengo, Besta amesema jengo la abiria limefikia asilimia 81, mnara wa kuongozea ndege asilimia 74, kituo cha zimamoto asilimia 88, vituo vya umeme asilimia 71 na jengo la huduma za hali ya hewa asilimia 87.
Amesema uwanja huo unajengwa kwa kiwango cha Daraja la 4E kwa kuzingatia viwango vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), ukiwa na njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa mita 3,600 na upana wa mita 45.
Besta amesema awamu ya kwanza ya uwanja huo itawezesha kuhudumia ndege kubwa aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba hadi abiria 350, huku uwanja ukiwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka.
Amesema mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), unalenga kuimarisha usafiri wa anga, kuongeza fursa za biashara, uwekezaji, utalii na usafirishaji wa mizigo, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.
Mhandisi Besta amesema mradi huo tayari umetoa ajira 9,059 kwa Watanzania, ambapo ajira 3,571 zimetolewa kupitia Package ya Kwanza na ajira 5,488 kupitia Package ya Pili, huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa 47.
Amewataka Watanzania, hususan wakazi wa Dodoma, kutumia fursa zitakazotokana na uwepo wa uwanja huo kwa kuanzisha na kukuza biashara zinazohitaji usafirishaji wa haraka wa bidhaa kama matunda, mboga mboga, samaki, kuku na maua, pamoja na kutumia fursa za utalii.
Katika hatua nyingine, Besta amesema TANROADS imechukua tahadhari kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na utabiri wa hali ya El Niño katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.
Amesema Wakala inaendelea kukagua barabara, madaraja, makaravati na mitaro, kusafisha mifumo ya kupitisha maji na kushughulikia maeneo yenye udhaifu ili kuimarisha usalama wa miundombinu wakati wa mvua kubwa.
Aidha, amewataka wananchi na watumiaji wa barabara kuchukua tahadhari kwa kuepuka kuvuka maeneo yaliyojaa maji, mito au madaraja yenye maji mengi na kutoa taarifa mapema wanapoona uharibifu wa miundombinu.
“Mvua ikiongezeka, tahadhari iongezeke,” amesema Besta.
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma kimefukia asilimia 89.02 kwa upande wa miundombinu, huku ujenzi wa majengo ukifikia asilimia 78.37 na ukitarajiwa kukamilika mwishoni mwa Disemba mwaka huu.






Comments
Post a Comment