Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Eliakim Maswi leo Septemba 25, 2026 ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wa Sekretarieti ya Mkoa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Bw. Maswi amesema ziara hiyo inalenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja katika utekelezaji wa miradi mikubwa inayolenga kuwaondoa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kujenga nyumba salama (Safe Houses) katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.Amesema Serikali imeelekeza fedha katika miradi hiyo kwa lengo la kuhakikisha watoto hao wanapata mazingira salama na huduma stahiki huku akieleza kuwa mpango huo pia unahusisha ujenzi wa Vituo vya Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) katika halmashauri 40 za za Kanda ya Ziwa.
Bw. Maswi amesema baada ya kubaini baadhi ya miradi kutokwenda kwa kasi iliyotarajiwa, wataalamu walitumwa kufanya ufuatiliaji na kutoa ushauri wa kitaalamu ikiwemo kuangalia maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa nyumba salama ambazo kwa mujibu wa mpango huo zinapaswa kujengwa katika maeneo yanayofaa na si kiholela.
Amesema pia ameamua kukutana na Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na viongozi wanaohusika na nyumba za kulelea watoto ili kujenga umiliki wa pamoja (ownership) na kuongeza uelewa wa viongozi kuhusu miradi hiyo.
“Tumekuja kukutana, kujadiliana na kuwakabidhi Makatibu Tawala miradi hii ili wajue ni miradi yao na wawe wasimamizi wake. Hata kama Wizara inajenga, miradi hii ipo katika ngazi za mikoa, hivyo ni muhimu viongozi wa mikoa kuifahamu na kuisimamia,”amesema Katibu Mkuu huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CP Salum Hamduni amesema wamekubaliana kuwa Bukumbi ni eneo linalofaa kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi hiyo kutokana na kuwa nje ya jiji na kuwa na mazingira yanayofaa kwa huduma zinazokusudiwa na ni eneo kubwa linalomilikiwa na Serikali.






Comments
Post a Comment