GEITA: Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira, amesema mamlaka hiyo imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wananchi, wawekezaji na watoa huduma kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma bora za nishati na maji katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Musira ameyasema hayo leo, Septemba 25, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la EWURA kwenye Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Amesema EWURA inatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu udhibiti wa huduma za nishati na maji, pamoja na kuwaeleza haki na wajibu wao kama watumiaji wa huduma hizo.
Kwa mujibu wa Musira, Kanda ya Ziwa inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Mara na Kagera, imeendelea kupewa elimu kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta zinazodhibitiwa na EWURA, pamoja na taratibu za kupata huduma na vibali.
Amesema moja ya maeneo yanayopewa msukumo ni uwekezaji katika vituo vya mafuta vijijini, ambapo EWURA imepunguza gharama za maombi na leseni kwa lengo la kurahisisha uwekezaji na kuongeza upatikanaji wa huduma za mafuta katika maeneo ya vijijini.
Musira amesema gharama ya maombi ya leseni kwa vituo vya mafuta vijijini imepunguzwa kutoka Shilingi 500,000 hadi Shilingi 50,000, huku ada ya leseni ya miaka mitano ikishuka kutoka Shilingi 1,000,000 hadi Shilingi 100,000.
Amesema hatua hiyo inalenga pia kupunguza utegemezi wa wananchi wa maeneo ya vijijini kwa wauzaji wa mafuta wasio rasmi, na kuhakikisha huduma ya mafuta inapatikana katika mazingira yanayosimamiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Katika eneo la nishati safi, Musira amesema EWURA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo nchini.
Aidha, amewahimiza wananchi kuchukua hatua za kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ili kuongeza upatikanaji wa maji na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa vipindi vya uhitaji mkubwa wa maji.
Musira amesema wananchi wanaokutana na changamoto katika huduma za nishati na maji wanaweza kuwasilisha kero na malalamiko yao EWURA ili yashughulikiwe kwa mujibu wa mamlaka na taratibu zilizowekwa.
“Tunataka wananchi wajue haki zao, wajue wanapoweza kupata huduma na pia wajue wapi pa kupeleka malalamiko pale wanapokutana na changamoto,” alisema Musira,
Amesema ushiriki wa EWURA katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa kuifikisha elimu na taarifa kwa wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali, huku akiwahimiza wakazi wa Geita na Kanda ya Ziwa kutembelea banda la EWURA ili kupata ufafanuzi kuhusu masuala yanayohusu huduma za nishati na maji.
Kwa upande wake, Afisa Mahusiano na Uhamasishaji wa EWURA, Tobietha Makafu, amewataka wakazi wa Geita na Kanda ya Ziwa kutembelea banda la mamlaka hiyo ili kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa.
Makafu amesema miongoni mwa huduma zinazopatikana katika banda hilo ni elimu kuhusu namna mafundi umeme wasio na leseni wanavyoweza kupata leseni na kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria.
Aidha, amesema wananchi na wawekezaji wanaweza kupata vipeperushi, miongozo na machapisho yenye taarifa kuhusu fursa za uwekezaji, ikiwemo uwekezaji katika vituo vya mafuta vijijini.
Ameongeza kuwa EWURA pia iko tayari kupokea kero na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za nishati na maji, ikiwemo malalamiko yanayohusu mamlaka za maji au TANESCO, pale ambapo wananchi hawajapata usikilizwaji wa kuridhisha.
Ushiriki wa EWURA katika maonesho hayo unaendelea kutoa fursa kwa wananchi na wadau kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu haki na wajibu wao, pamoja na taratibu za kupata huduma na vibali katika sekta zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.



Comments
Post a Comment