Kutokana na tahadhari kuhusu uwezekano wa mvua kubwa za El Niño, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limefanya marekebisho ya ratiba ya mitihani na upimaji wa kitaifa iliyokuwa ifanyike katika miezi ya Oktoba na Novemba 2026.
Akizungumza leo, Ijumaa, Septemba 25, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Wanu Hafidh Ameir, amesema uamuzi huo umefanyika kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani.
Amesema licha ya Wizara kupokea taarifa kutoka mikoa mbalimbali kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, imeona umuhimu wa kufanya marekebisho ya ratiba ya uendeshaji wa Upimaji na Mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026.
“Lengo la marekebisho ya ratiba ni kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka za mitihani iwapo mvua kubwa zitatokea mwezi Novemba 2026,” amesema.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026, badala ya Oktoba 21 na 22.
Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili, uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 17 na 18, sasa utafanyika Oktoba 7 na 8, 2026.
Kwa upande mwingine, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 2 hadi 13, sasa utafanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23, 2026.
Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, ambao awali ulipangwa kuanza Novemba 9 hadi 27, sasa utaanza Oktoba 19 na kumalizika Novemba 6, 2026.

Comments
Post a Comment