WACHIMBAJI WADOGO GEITA KUPATIWA ELIMU YA KEMIKALI
Na Mwandishi wetu
SERIKALI imesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Sekta ya Madini na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni wa lazima na si wa hiari, kutokana na matumizi makubwa ya kemikali katika shughuli zote za uchimbaji.
Akizungumza Leo Septemba 24,2026 katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita wakati wa maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolokia ya madini Waziri,Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira na Mahusiono,Deus Clement Sangu amesema kemikali kama Zebaki na Cyanide ndizo zinazoendesha sekta ya dhahabu, lakini zisipodhibitiwa zinaweza kuwa janga kwa afya ya binadamu, hasa kwa vijana wanaofanya kazi migodini bila mavazi kinga.
Amesema hatua za Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kudhibiti na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya kemikali hizo ni matokeo chanya ambayo yanaendana moja kwa moja na Nguzo Namba 2 ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kumwezesha Mtanzania kiuchumi na kijamii.
"Ni lazima tuwafikie wachimbaji wetu wadogo wa hapa Geita na Bukombe. Hawahitaji tu leseni, wanahitaji elimu. Kijana akipata ajira mgodini lakini akapoteza maisha kwa sumu ya kemikali, tumepoteza nguvukazi ya Taifa," alisisitiza.
Aidha, amesema majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira kupitia OSHA, amesema ulinzi wa afya na usalama kazini ndio msingi wa nchi kufikia malengo yake ya kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amemalizia kwa kuitaka Ofisi ya Mkemia Mkuu kuongeza kasi ya utoaji elimu mashinani ili madini ya Geita yanufaie kizazi cha sasa bila kuua kizazi cha kesho.
Mwisho



Comments
Post a Comment