SERIKALI imeeleza dhamira ya kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi za wananchi, usalama wa mifumo ya kidijitali na mapambano dhidi ya uhalifu wa mtandao kupitia hatua ya kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Usalama wa Mtandao na Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa mwaka 2014, maarufu kama Mkataba wa Malabo.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, ameeleza hayo leo, Novemba 5, 2026, Bungeni jijini Dodoma, Akiwasilisha Azimio la kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika wa usalama wa Mtandao na ulinzi wa Taatifa Binafsi wa Mwaka 2014(Mkataba wa Malabo) ili kuimarisha mifumo ya kisheria na kiutendaji katika kulinda taarifa binafsi na kuhakikisha usalama wa huduma za kidijitali nchini.
Amesema kuridhiwa kwa mkataba huo kutaimarisha usimamizi wa ukusanyaji, matumizi, uhifadhi na uchakataji wa taarifa binafsi, kwa kuzingatia misingi ya ridhaa, uhalali, uwazi, usahihi na usalama wa taarifa hizo. Hatua hiyo pia itasaidia kuzuia matumizi ya taarifa za watu kinyume cha sheria na kulinda haki za wananchi katika mazingira ya kidijitali.
Waziri Kairuki, amesema mkataba huo unasisitiza haki ya mtu kupata taarifa zake, kuzirekebisha au kuomba zifutwe pale inapostahili, pamoja na kupinga uchakataji wake usiozingatia sheria. Aidha, unaweka msingi wa kuwepo kwa mamlaka huru za kitaifa zitakazosimamia ulinzi wa taarifa binafsi na kuwawajibisha wanaokusanya au kuchakata taarifa hizo.
Katika eneo la usalama wa mtandao, amesema mkataba unaweka misingi ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa kimtandao, ikiwemo kuingia kwenye mifumo ya kompyuta bila ruhusa, kuiba au kubadilisha taarifa, kuharibu mifumo na kutumia taarifa zilizopatikana kinyume cha sheria.
Ameongeza kuwa kuridhiwa kwa mkataba huo kutaimarisha ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika na jumuiya za kimataifa katika kubadilishana taarifa, kufanya uchunguzi na kushirikiana katika kuwachukulia hatua wahusika wa uhalifu wa mtandao unaovuka mipaka ya nchi.
"utekelezaji wa mkataba huo unatarajiwa kuongeza imani ya wananchi katika matumizi ya huduma za kidijitali, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ubunifu, pamoja na kuiwezesha Tanzania kuendana na viwango vya kikanda na kimataifa katika masuala ya usalama wa mtandao na ulinzi wa taarifa binafsi". Amesema
Kadhalika, Waziri Kairuki amebainisha kuwa Tanzania tayari ina sheria zinazohusiana na maeneo hayo, zikiwemo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2015, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022, Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 pamoja na Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019.
"kuridhiwa kwa Mkataba wa Malabo kutasaidia kuimarisha utekelezaji wa mifumo hiyo ya kisheria na kuipa Tanzania nafasi nzuri zaidi ya kushirikiana na mataifa mengine katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na maendeleo ya teknolojia". Amesema
Hoja hiyo imewasilishwa kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayolipa Bunge mamlaka ya kujadili na kuridhia mikataba inayohitaji idhini yake.

Comments
Post a Comment