WAZIRI wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuimarisha uwekezaji na uzalishaji ili ndani ya miaka mitatu liweze kufikia kiwango cha kushindana na kampuni kubwa za uchimbaji madini nchini, zikiwemo Barrick, Geita Gold Mine na Shanta.
Mavunde ametoa changamoto hiyo Novemba 7, 2026, wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha Nishati Safi cha Rafiki Briquettes kilichopo Chigongwe, mkoani Dodoma, akieleza kuwa STAMICO ina rasilimali na fursa nyingi zinazopaswa kutumiwa kuifanya kuwa taasisi imara na yenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.
Amesema STAMICO imepiga hatua kubwa katika kuimarisha utendaji wake, ikilinganishwa na hali ya miaka mitano iliyopita ambapo shirika hilo lilikuwa katika changamoto za kifedha na kutegemea ruzuku ya Serikali. Kwa mujibu wa Mavunde, mapato ya shirika yameongezeka kutoka Shilingi bilioni moja hadi zaidi ya Shilingi bilioni 89 chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Venance Mwasse.
Ameeleza kuwa shirika hilo linaendelea kupanua uwekezaji katika miradi ya dhahabu Kigosi, madini adimu katika Vilima vya Wigu mkoani Morogoro, pamoja na nikeli katika maeneo ya Ntaka na Chingwea, akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo ili kuimarisha uzalishaji na mapato.
Akizungumzia matumizi ya nishati safi, Mavunde amesema uwekezaji wa kiwanda cha Rafiki Briquettes unaunga mkono azma ya Serikali ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034, kwa kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Aidha, ameitaka STAMICO kutumia ipasavyo rasilimali za makaa ya mawe zilizopo katika Mgodi wa Kiwira kwa kushirikiana na wawekezaji kuzalisha nishati ya umeme. Amesema mgodi huo una akiba inayoweza kusaidia uzalishaji wa tani milioni moja za makaa ya mawe kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 80, hatua inayoweza kuchangia kufikia malengo ya taifa ya kuongeza uzalishaji wa umeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amesema gharama ya Mradi huo wa Rafiki Briquettes ni Shilingi bilioni 3.7 na kina uwezo wa kuzalisha tani 20 za nishati safi kwa saa, huku kikitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa takribani watu 100, wengi wao wakiwa vijana.
Dkt. Mwasse amesema kiwanda hicho ni sehemu ya mkakati wa STAMICO kuongeza thamani ya makaa ya mawe kwa kuyatumia kuzalisha nishati safi, akibainisha kuwa teknolojia hiyo imewezesha kuanzishwa kwa viwanda vingine vitano vinavyohusiana na uzalishaji wa nishati hiyo nchini.
Ameongeza kuwa STAMICO inaendelea na maandalizi ya kukamilisha kiwanda kingine mkoani Geita na kuanzisha ujenzi wa kiwanda cha Tanga katika mwaka huu wa fedha. Amesema uwekezaji huo hautatoa ajira pekee, bali pia utafungua fursa za biashara katika usafirishaji, huduma za chakula, usambazaji wa vipuri na huduma nyingine zitakazowanufaisha wananchi, hususan vijana na wanawake.
Dkt. Mwasse amesema jumla ya gharama za vifaa na miradi iliyozinduliwa katika hafla hiyo ni Shilingi bilioni 6.09, ikiwemo mitambo ya uchimbaji wa madini, magari na mashine nyingine zinazolenga kuongeza uwezo wa shirika katika utekelezaji wa majukumu yake.
Katika kuimarisha uhusiano na jamii inayozunguka mradi huo, STAMICO imeahidi kujenga shule ya sekondari katika eneo la Chigongwe ambapo watanza na darasa moja huku Waziri wa Madini Mhe. Mavunde na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini wakichangia tofali 5,000 kwa ajili ya ujenzi wa darasa jingine.
"Nasisitiza umuhimu wa upandaji miti na matumizi ya nishati safi katika kulinda mazingira eneo hili la chigongwe". Amesisitiza
Uzinduzi wa kiwanda hicho ni sehemu ya juhudi za STAMICO kupanua wigo wa uwekezaji, kuongeza thamani ya rasilimali za madini na kuchochea upatikanaji wa nishati safi, sambamba na kufungua fursa za ajira na biashara kwa wananchi.






Comments
Post a Comment