MBUNGE wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mheshimiwa Mwita Waitara, amehoji Serikali kuhusu hatua na muda wa kupeleka vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyokamilika kujengwa katika maeneo ya vijijini ya Mtaa, Umera, Magoma na Yuyahanja, ili wananchi waanze kunufaika na huduma za afya katika maeneo yao.
Akizungumza Bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu Leo Novemba 3,2026, Mheshimiwa Waitara amesema kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya vituo vya afya pekee hakutoshi kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, bali kunahitajika pia vifaa tiba na wataalamu wa afya watakaowezesha utoaji wa huduma hizo.
Amesisitiza kuwa wananchi wamekuwa wakisubiri kwa hamu vituo hivyo kuanza kutoa huduma, hivyo ni muhimu Serikali kuhakikisha vifaa tiba vinapelekwa kwa wakati ili majengo hayo yaweze kutumika kwa lengo lililokusudiwa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya Dkt.Florence Samizi amesema Serikali inatambua umuhimu wa hatua hiyo, akieleza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya afya, hatua inayofuata ni kuhakikisha vinapatiwa wataalamu pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema Ofisi za Mikoa na Halmashauri zinaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Wizara ya Afya katika kuratibu upatikanaji wa vifaa tiba, huku Bohari ya Dawa (MSD) ikiendelea na mchakato wa kusambaza vifaa hivyo katika vituo vya afya vilivyokamilika nchini.

Comments
Post a Comment