Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara, amesema amesikitishwa na wizi na matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma zilizobainishwa katika baadhi ya miradi na taasisi za Serikali kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akitaka watendaji waliohusika kuwajibishwa.
Akichangia taarifa za Kamati za Bunge kuhusu ripoti za CAG, Novemba 3, 2026, jijini Dodoma, Waitara amesema ukaguzi huo umebainisha changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi ya fedha yasiyozingatia taratibu, mapungufu katika mikataba na manunuzi, pamoja na malipo yanayohitaji ufafanuzi kutoka kwa watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za umma.
Amesema miongoni mwa maeneo yanayohitaji ufuatiliaji ni Mlimani City, ambako kuna hoja zinazohusu usimamizi wa mapato, ulipaji wa kodi na utekelezaji wa mikataba, akitaka Serikali kuweka wazi namna eneo hilo linavyosimamiwa na kuhakikisha mapato yanayostahili yanakusanywa kwa mujibu wa sheria.
“Ukiangalia Mlimani City, kuna maswali kuhusu mapato na kodi. Hata mkataba ukiisha, haieleweki wazi utaratibu wa umiliki na usimamizi utakavyokuwa. Sasa tunajiuliza, tunakwenda wapi?” amehoji Waitara.
Katika sekta ya michezo, Waitara amesema ripoti ya CAG imeibua hoja kuhusu matumizi ya fedha katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo, akivitaja viwanja vya Arusha, Benjamin Mkapa na Uhuru kuwa miongoni mwa miradi inayohitaji maelezo ya kina kuhusu gharama, taratibu za manunuzi na usimamizi wa utekelezaji wake.
Amesema katika mradi wa Uwanja wa Arusha, ripoti imeonesha ongezeko la gharama kutoka makadirio ya awali ya Shilingi bilioni 187 hadi Shilingi bilioni 338.54, sambamba na hoja kuhusu taratibu za manunuzi na usimamizi wa mradi huo.
Aidha, ameeleza kuwa katika ukarabati wa viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru, kuna hoja zinazohusu gharama za zabuni, malipo ya kazi na udhibiti wa ubora, hivyo kuitaka Serikali kutoa ufafanuzi na kuhakikisha mapendekezo yaliyotolewa na CAG yanatekelezwa.
Waitara amesisitiza kuwa hoja zake hazilengi kupinga ubora wa viwanja hivyo wala mafanikio ya Tanzania katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, bali zinahusu uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za walipa kodi.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema viwanja vinavyotumika katika mashindano ya kimataifa hukaguliwa na mamlaka husika, akibainisha kuwa Uwanja wa Arusha ni miongoni mwa viwanja vinavyokidhi viwango vya FIFA.
Makonda amesema hatua iliyofikiwa katika miundombinu ya michezo ni sehemu ya mafanikio yaliyowezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.
Hata hivyo, Waitara amesisitiza kuwa kutambuliwa kwa ubora wa uwanja hakupaswi kuondoa umuhimu wa kujibu hoja za ukaguzi kuhusu matumizi ya fedha zilizotumika katika ujenzi wake.
“Sikatai ubora wa uwanja, bali nachokataa ni matumizi mabaya ya fedha katika uwanja huo,” amesisitiza.
Serikali imetakiwa kuhakikisha viongozi na watendaji wote waliopewa dhamana ya kusimamia fedha za umma wanawajibika ipasavyo, wakizingatia uadilifu na kuhakikisha uwekezaji unaofanywa unaleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi badala ya kuacha maswali na hoja za ukaguzi zinazojirudia.

Comments
Post a Comment