Kamati Huru ya Wazo Bunifu imeanza hatua ya mwisho ya tathmini ya mawazo bunifu kwa kufanya mahojiano ya ana kwa ana na wabunifu 60 waliofuzu, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kusaka mawazo bora yatakayosaidia kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bi. Zawadia Nanyaro, amesema kamati imejipanga kuwapa washiriki fursa ya kueleza kwa kina msingi wa mawazo yao, namna yanavyoweza kutekelezwa na mchango wake katika kuimarisha utendaji wa TRA.
Bi. Nanyaro amewataka wabunifu hao kujiamini na kuwa huru wakati wa mahojiano ili kuiwezesha kamati kupata uelewa mpana wa kila wazo na kufanya tathmini ya kina kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
Zoezi hilo lilianza kwa kamati kutathmini jumla ya mawazo 9545 yaliyopokelewa na kuchakatwa kwa umakini. Hatua hii ya sasa inatarajiwa kufanyika kwa siku sita, ambapo kamati itakuwa ikifanya mahojiano na wabunifu 10 kila siku, hatua itakayowezesha uchambuzi wa kina wa mawazo na kubaini yale yenye tija zaidi kwa Mamlaka.
Kupitia mchakato huo, washindi 20 wanatarajiwa kupatikana na kujishindia zawadi mbalimbali, huku mshindi wa kwanza akitarajiwa kujinyakulia shilingi milioni 50. Mawazo yatakayochaguliwa yanatarajiwa kutumiwa na TRA katika kuboresha huduma, kupanua wigo wa kodi na kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali.




Comments
Post a Comment